Simba SC

Simba SC Yaiva Mbadala wa Mwalimu, Kumsajili Mshambuliaji Huyu Hatari!

Vardo August 12, 2026 10:32 am

Uongozi wa Simba SC umeamua kugeuza machungu ya kukosa saini ya mshambuliaji Selemani Mwalimu kuwa fursa ya kusajili mashine mpya ya mabao, kufuatia mchezaji huyo kujiunga na watani wao wa jadi, Yanga SC.

Mwalimu, ambaye alikuwa kwenye rada za Wekundu wa Msimbazi kwa muda mrefu, ameibukia Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Wydad AC ya Morocco—klabu inayommiliki hadi Juni 30, 2029.

Hata hivyo, badala ya kukaa na kulalamika, viongozi wa Msimbazi wameanza kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha safu yao ya ushambuliaji inaimarishwa mapema kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

Taarifa za ndani kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Simba SC inaendelea kutazama chaguo mbalimbali za wachezaji wenye uzoefu, huku jina la mshambuliaji mzawa likitajjwa kushika kasi.

“Dirisha la usajili bado liko wazi. Miongoni mwa wachezaji wazawa tunaoshughulikia mchakato wao ni Mgunda, lakini mashabiki watarajie sapraizi kubwa zaidi kabla ya usajili kufungwa,” kilieleza chanzo hicho cha ndani.

Mgunda si jina ngeni kwenye masikio ya wapenzi wa soka nchini. Msimu uliopita akiwa na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alifanikiwa kufunga mabao mawili, huku msimu wa 2023/24 akiwa na Singida Black Stars akitikisa nyavu mara sita.

Ili kufanikisha mpango huo, Simba itapaswa kuingia makubaliano na klabu ya Mashujaa FC, ambapo Mgunda bado ana mkataba wa mwaka mmoja unaombana.

Ujio wa mshambuliaji mpya ndani ya Msimbazi unatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji, huku presha kubwa ikiwa kwa viongozi kuona kama watajibu mapigo ya Yanga kabla ya dirisha kufungwa.

Sababu za Simba Kukosa Saini ya Selemani Mwalimu na Kutua Yanga Zafichuka