Kocha wa Mashujaa FC Afunguka Maandalizi ya Ligi Kuu, Mbinu na Majeruhi
Wakati Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027 ikianza rasmi leo, Kocha wa Mashujaa FC, Aman Josiah, ameweka wazi maandalizi ya kikosi chake huku akibainisha kuwa mastaa wake wameanza kuelewa na kuingia kikamilifu kwenye mfumo wake wa mbinu.
Josiah, ambaye amejiunga na Mashujaa FC msimu hii akitokea Dodoma Jiji—ambayo aliisaidia kumaliza katika nafasi ya tisa msimu uliopita—amesema mechi saba za kirafiki walizocheza zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuwajenga wachezaji kimbinu na kutengeneza muunganiko mzuri kati ya wachezaji wapya na wale wa zamani.
“Kwa maandalizi tuliyofanya na mechi tulizocheza, morali ipo juu sana kwa wachezaji. Pia maelekezo yangu wanayafuata vizuri, hivyo nina imani kubwa kuwa tutafanya vyema msimu huu,” amesema kocha Josiah.
Hali ya Majeruhi Kikosini
Akizungumzia kuhusu majeruhi ndani ya kikosi chake, Josiah amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kwa kueleza kuwa kina kikosi mpana kinachoweza kukabiliana na changamoto yoyote. Pia alimtaja kiungo Mundhir Vuai kuwa tayari anarejea taratibu mazoezini.
“Majeruhi wapo na wanaendelea kupona. Mfano Mundhir Vuai tayari yupo nami mazoezini. Kikubwa ni kwamba waliopo wapo tayari, wana afya njema na wana utayari wa kupambana,” aliongeza.
Mashujaa FC itaanza kibarua chake cha Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027 kwa kumenyana na Coastal Union siku ya Jumamosi, Agosti 15, 2026, katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.