Oscar Mwajanga Mbeya City
Michezo Bongo

Oscar Mwajanga Aweka Wazi Vita ya Mabao Mbeya City, Acha Ujumbe Mzito

Vardo August 30, 2026 7:50 am

Mwajanga, ameweka wazi kuwa licha ya kiwango bora anachoendelea kukionyesha kikosini humo, lengo lake kuu ni kuhakikisha anavuka rekodi yake ya mabao aliyoiweka msimu uliopita wa 2025-2026.

Nyota huyo aliyetua Mbeya City msimu huu wa 2026-2027 akitokea Tanzania Prisons iliyoshuka daraja hadi Championship, amekuwa nguzo muhimu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kutokana na mchango wake mkubwa uwanjani.

Akizungumza kuhusu mwenendo wake, Mwajanga alisema mshambuliaji mzuri anapimwa kwa idadi ya mabao aliyofunga, na yeye yupo tayari kutimiza hilo licha ya ushindani mkali wa namba kutoka kwa nyota wenzake.

“Licha ya ushindani uliopo, nitaendelea kuonyesha kipaji changu kadri nitakavyopata nafasi ya kucheza. Jambo zuri tayari nimeshaanza vizuri kwa dakika ninazopewa, lengo ni kuendelea kufanya vizuri na kuepuka presha kama ya msimu uliopita,” alisema Mwajanga.

Aidha, aliongeza kuwa kutopata nafasi ya kuanza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza hakuwezi kumvunja moyo, bali kunampa chachu ya kuendelea kumshawishi kocha kwa kila dakika anayopewa.

“Kila mchezaji ana nafasi ya kucheza kutokana na mahitaji ya timu. Ninachokifanya ni kutoa kilicho bora bila kujali nimeanza kikosi cha kwanza au nimetokea benchi, kwani lengo letu sote ni kuipambania Mbeya City,” aliongeza.

Tangu ajiunge na Mbeya City msimu huu, Mwajanga tayari amehusika kwenye mabao manne ya timu hiyo katika Ligi Kuu Bara (akifunga mabao 3 na kutoa pasi 1 ya bao), takwimu zinazomfanya kuwa mshambuliaji kinara kikosini hapo.

Dabo Aibuka na Kumjuza Mbinu Toure ya Kutoboa Yanga na Ligi Kuu Katwila Aainisha Mipango Geita Gold: “Bukombe Kitakuwa Mwiba”