Ibrahim Doumbia Simba SC
Simba SC

Mchambuzi Afichua Sababu Doumbia Kukwama Simba SC

Vardo September 2, 2026 8:01 pm

Mshambuliaji mpya wa Simba SC, Ibrahim Doumbia, anaendelea kuweka mjadala mzito miongoni mwa mashabiki na wachambuzi wa soka nchini kuhusu namna bora ya kutumika kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Mchambuzi wa soka nchini, Godlisten Muro, amebainisha kuwa changamoto kuu inayomkabili mshambuliaji huyo si kukosa kiwango au uwezo wa kufunga, bali ni namna anavyoshindwa kuingiana na mfumo wa sasa unaotumiwa na Simba SC.

Doumbia alitua Msimbazi akitokea klabu ya AS Korofina ya nchini Mali akiwa na muendelezo mzuri wa ufungaji, baada ya kumaliza msimu uliopita akiwa kinara wa mabao nchini humo na kufumania nyavu mara 17. Hata hivyo, katika mechi zake tano za kwanza za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, hajaweka mpira wowote nyavuni wala kutoa pasi ya bao (assist), jambo lililoongeza presha kubwa kwake.

Doumbia vs Mfumo wa Simba

Muro anaeleza kuwa tatizo la Doumbia linatakiwa kutazamwa zaidi kwenye mfumo wa timu na ushirikiano wake na wachezaji wengine wa safu ya ushambuliaji.

“Ukiwaona wachezaji kama Libasse Gueye na Anicet Oura, unaona mtiririko mzuri na kasi ya timu. Lakini akishacheza Doumbia, anaweza kuilazimisha timu kubadili mfumo wake ili kuendana naye,” alisema Muro.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa Muro, Simba imejengwa katika msingi wa mpira wa kasi, pasi za haraka, na miondoko ya wachezaji wa eneo la mbele. Mfumo huu unahitaji mshambuliaji anayeweza kushirikiana na wenzake kujenga mashambulizi badala ya kusubiri mpira wa mwisho eneo la hatari.

“Timu yenye wachezaji wenye kasi eneo la juu inahitaji mtu anayeweza kukamilisha mzunguko (circuit) wa mashambulizi kwa pamoja. Ndiyo maana Libasse, Oura na Elie Mpanzu wanaelewana kwa urahisi kwa sababu wanatengeneza muunganiko unaoendana kimfumo,” aliongeza.

Kazi ipo kwa Doumbia Badala ya Simba

Muro anasisitiza kuwa suluhisho la kudumu si Simba kubadilisha mfumo wake mzima ili kumbeba Doumbia, bali ni jukumu la mshambuliaji huyo kuzoea na kuingia kwenye mfumo uliopo.

“Ni ngumu sana kwa timu kubadilisha mfumo wake ili kumridhisha mchezaji mmoja. Mchezaji ndiye anayepaswa kupambana kuingia kwenye mfumo wa timu.”

Hata hivyo, Muro amewatake mashabiki kutomkatia tamaa nyota huyo, akieleza kuwa ukame wa mabao haumaanishi kuwa amepoteza uwezo wake wa soka:

“Inawezekana ikawa si mbaya kwake wala kwa Simba. Tatizo kuu ni kutolingana kwa mtindo wa uchezaji. Ni mchezaji mzuri, lakini kwa sasa yupo nje ya matarajio ya kimfumo.”

CAF Yairidhia MOI Tiba za Michezo AFCON 2027 Yanga Yachukua Hatua Nzito kwa Job na Mzize: Kupelekwa Afrika Kusini Kwa Vipimo Zaidi