MOI AFCON 2027
Habari za michezo

CAF Yairidhia MOI Tiba za Michezo AFCON 2027

Vardo September 2, 2026 7:53 pm

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeeleza kuridhishwa na maandalizi na uwezo wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika kutoa huduma za afya na tiba za michezo kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Fainali hizo za kihistoria zinatarajiwa kuandaliwa kwa pamoja na nchi tatu za Afrika Mashariki: Tanzania, Kenya na Uganda.

Kauli hiyo ya pongezi imetolewa kufuatia ziara ya ujumbe wa wataalamu wa afya kutoka CAF uliotembelea MOI. Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa ni kutathmini miundombinu, uwezo wa kiufundi na rasilimali watu za taasisi hiyo katika kuhudumia majeraha ya mifupa, mishipa ya fahamu na dharura zitakazojitokeza wakati wa mashindano.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja wa Huduma za Afya wa CAF, Boubakary Sidiki, alipongeza jitihada zinazofanywa na MOI na kusisitiza umuhimu wa huduma za tiba kwenye michezo.

“Huduma bora na za kisasa za afya ni nguzo kuu ya kuhakikisha usalama, afya na ustawi wa wanamichezo wakati wote wa mashindano makubwa kama AFCON,” alisema Sidiki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa MOI, Dk. Asha Abdullah, alibainisha kuwa taasisi hiyo ipo tayari kutumia utaalamu wake wa hali ya juu kushirikiana na CAF pamoja na wadau wote wa michezo ili kuhakikisha nchi inakuwa na mfumo imara na thabiti wa tiba za michezoni.

“MOI iko tayari kikamilifu kushirikiana na CAF na wadau wote kuelekea AFCON 2027. Tunaamini maandalizi haya ni fursa pekee ya kuimarisha sekta ya tiba za michezoni nchini na kuhakikisha wanamichezo wanapata huduma bora, salama na kwa wakati stahiki,” alieleza Dk. Asha.

Yakoub Suleiman Afunguka Majeraha Yake Simba, Ataja Tarehe ya Kurejea Uwanjani! Mchambuzi Afichua Sababu Doumbia Kukwama Simba SC