Yanga vs Gaborone United
Yanga SC

Siri Yafichuka! Sababu ya Mzize na Job Safarini Botswana Huku Hawachezi Dhidi ya Gaborone Utd

Vardo September 2, 2026 9:24 am

Uongozi wa klabu ya Yanga umeweka wazi kuwa beki Dickson Job na mshambuliaji Clement Mzize hawatakuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani kuwakabili Gaborone United katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hatua hiyo imekuja licha ya nyota hao wawili kuonekana kwenye msafara wa timu hiyo ulioondoka nchini jana kuelekea Botswana. Yanga itarushana roho na Gaborone United siku ya Jumamosi, Septemba 5, 2026, kuanzia saa 2:00 usiku katika mchezo huo wa kusaka nafasi ya kutinga hatua inayofuata.

Ukweli Kuhusu Safari Yao Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amefafanua kuwa Job na Mzize hawakusafiri moja kwa moja kwa ajili ya mchezo huo, bali wataishia Afrika Kusini kufanyiwa vipimo vya mwisho vya kitabibu (final medical checkup) kabla ya kuruhusiwa kurejea uwanjani.

“Dickson Job na Clement Mzize hawatakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga huko Gaborone. Wataishia Afrika Kusini kwa ajili ya vipimo vya mwisho ili kuthibitisha utayari wao wa kimwili,” alisema Kamwe.

Klabu Yakataa Kuharakisha Urejeo Wao Kamwe alieleza kuwa ingawa wachezaji hao wanaonekana kufanya vizuri na kukimbia bila shida mazoezini, Yanga haitaki kufanya maamuzi kwa kutazama kwa macho pekee bila kufuata ushauri wa kitaalamu.

“Tumeshawaona na kujadili, wanakimbia vizuri mazoezini lakini hatutaki kutegemea macho tu. Tunataka tufuate taratibu zote za kitaalamu. Ndio maana tumeingia gharama ya kuwasafirisha hadi Afrika Kusini walikotibiwa ili wakakutane na madaktari bingwa waliowatibu,” aliongeza Kamwe.

Kurejea Uwanjani Mwezi Oktoba Baada ya vipimo hivyo, wachezaji hao wanatarajiwa kurejea nchini kuendelea na mazoezi na wenzao, huku tarehe rasmi ya kurejea kwenye mechi ikitegemea majibu ya madaktari na tathmini ya benchi la ufundi.

Akimalizia, Ali Kamwe aliwatoa hofu mashabiki wa Wananchi kwa kusema: “Mkiwaona kwenye safari msidhani wanakwenda kushuhudia Wabotswana. InshaAllah mwezi wa kumi (Oktoba) wanaweza kuanza kazi rasmi na timu.”

Kawempe Muslim Ladies Mabingwa CECAFA: Watavunja Mwiko Ligi ya Mabingwa Afrika? Vita ya Clean Sheets: Kassali na Diarra Watengeneza Rekodi Ligi Kuu