Nahodha Pamba Jiji Aweka Wazi Kilichowaponza Ligi Kuu, Aapa Kuichapa JKT Tanzania
Mfululizo wa mechi nne bila kupata ushindi ndani ya Ligi Kuu ya NBC umeamsha hisia mpya ndani ya kikosi cha Pamba Jiji, huku wachezaji wa timu hiyo wakitaja sababu zilizowakwaza na kutangaza rasmi kuwa muda wa kuteseka umewadia mwisho.
Pamba Jiji, ambayo ilionyesha kiwango bora msimu uliopita, haijaanza vyema msimu huu licha ya kuwa na kikosi chenye wachezaji wenye uwezo mkubwa wa mmoja mmoja. Katika michezo hiyo nne, wamefanikiwa kuondoka na pointi moja pekee, wakipoteza mechi tatu mfululizo na kuruhusu mabao saba huku wakifunga mabao matatu, hali inayowafanya washikilie nafasi ya 14 kwenye msimamo.
Safari yao ya msimu huu ilianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji nyumbani, kabla ya kukutana na pigo la kufungwa 2-1 na Simba SC uwanjani CCM Kirumba Mwanza. Baadaye walikubali kichapo kingine cha mabao 2-1 ugenini dhidi ya Azam FC na kutimishwa na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mabingwa Watetezi, Yanga SC.
Akizungumzia mwenendo huo, Nahodha wa Pamba Jiji, Hassan Kibailo, ameeleza kuwa ratiba ya mapema imewakutanisha na timu zenye uzoefu na uwezo mkubwa, lakini kwa sasa wanajipanga upya kurejesha furaha kwa mashabiki wao.
“Tumeanza na vigogo ambao wametuzidi kwa vitu kadhaa, lakini tunapoenda kukutana na timu za saizi yetu lazima tupambane kwa jasho na damu ili kupata pointi tatu. Tutaanza na JKT Tanzania na hii itakuwa zamu yetu kushangilia,” alisema Kibailo.
Nahodha huyo aliongeza kuwa, licha ya matokeo hayo mabaya, timu hiyo imekuwa na wastani mzuri wa kufunga katika kila mechi kasoro dhidi ya Yanga. Hata hivyo, amesisitiza kuwa eneo la ulinzi linahitaji umakini mkubwa ili kuzuia makosa yanayogharimu timu.