Simba SC vs Mighty Wanderers
Simba SC

Simba SC Yaonyesha Meno Ligi ya Mabingwa: “Hatuendi Malawi Kutafuta Sare!”

Vardo September 3, 2026 12:42 pm

Klabu ya Simba SC imeweka wazi msimamo na dhamira yake kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi, ikisisitiza kuwa haitakwenda ugenini kujilinda wala kutafuta sare, bali kusaka pointi tatu muhimu.

Wekundu wa Msimbazi wanatarajiwa kushuka dimbani nchini Malawi siku ya Jumapili, Septemba 6, huku msafara wa timu hiyo ukitarajiwa kuondoka nchini kesho, Ijumaa, Septemba 4.

Kasi Ongezeka Mazoezini

Baada ya kukamilisha ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ushindi dhidi ya Golden Glitters, benchi la ufundi la Simba limeongeza kasi ya maandalizi ili kurekebisha makosa na kuongeza makali kabla ya pambano hilo la kimataifa.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ameeleza kuwa timu imerejea uwanjani kwa lengo la kusahihisha mapungufu yote yaliyoonekana katika michezo iliyopita.

“Baada ya kumaliza mchezo wetu wa Ligi Kuu dhidi ya Golden Glitters, tumerudi tena mazoezini kuboresha palipokuwa na mapungufu. Mchezo dhidi ya Mighty Wanderers ni mgumu kwa sababu unapocheza na mabingwa wa nchi husika katika Ligi ya Mabingwa Afrika, haiwezi kuwa mechi nyepesi,” alisema Ahmed Ally.

Vita ya Dakika 90 za Ugenini

Ahmed amesisitiza kuwa msimamo wa Simba ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ugenini ili kujitengenezea mazingira mazuri kuelekea mchezo wa marudiano utakaopigwa jijini Dar es Salaam.

“Lengo letu kuu ni kupata ushindi ugenini. Hatuendi Malawi kutafuta sare wala kufungwa mabao uchache—tunakwenda kupambana kwa ajili ya ushindi. Tumesalia na siku chache za maandalizi ya mwisho, na kwa ubora wa kikosi tulicho nacho, tuna imani kubwa ushindi utapatikana, InshaAllah,” aliongeza Ahmed.

Yanga Yanoa Makali Botswana: Walter Halson Afichua Mpango wa Gaborone United Mngqithi Anza Kazi Yanga: Awasoma Gaborone United Kuelekea Mchezo wa Ligi ya Mabingwa