Clatous Chama Simba SC
Simba SC

Chama Afunguka Siri Nzito: “Nilijutia Kuisaliti Simba na Kujiunga na Yanga”

Vardo September 6, 2026 8:48 am

Kiungo mchezeshaji wa Simba SC, Clatous Chama, hatimaye amevunja ukimya na kufunguka kwa mara ya kwanza kuhusu safari yake ya kumpiga chenga za maisha Msimbazi, kujiunga na watani wao wa jadi Yanga SC, kuelekea Singida Black Stars, na hatimaye kurejea tena nyumbani Simba.

Chama ameweka wazi kuwa kipindi alichokaa nje ya klabu hiyo kilikuwa na mafunzo makubwa katika maisha na maamuzi yake ya soka.

Usiku wa Simanzi Baada ya Kusaini Yanga Akiizungumzia siku aliyoweka saini kujiunga na Yanga SC, Chama amekiri kuwa haukuwa uamuzi mwepesi na alijikuta akiijutia hatua hiyo kabla hata hajaanza kuitumikia rasmi klabu hiyo.

“Kuhama Simba kwangu nilijutia sana. Hata siku ile niliposaini mkataba, haukuwa usiku wa amani kwangu. Lakini ilikuwa ni hali tuliyopaswa kuikabili kwa wakati huo,” alisema Chama.

Aliongeza kuwa moyo wake ulikuwa bado Msimbazi na viongozi wa Simba walikuwa wanatambua vyema hamu yake ya kuendelea kuvaa jezi ya Msimbazi.

Simu ya Rais Mo Dewji Kutoka Dubai Baada ya kuweka saini Yanga, matumaini ya Chama kurejea Simba yaliibuka tena siku iliyofuata baada ya kupokea simu kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’, ikimtaka wakutane nchini Dubai.

“Nilikuwa na uwezo wa kugoma kwenda kwa sababu tayari nilikuwa nimeshasaini Yanga, lakini kwa heshima ya Simba nililazimika kusafiri kutoka Zambia hadi Dubai kumpokea Rais. Tulikaa na kuzungumza kwa kirefu ili kutafuta namna ya kutengua uamuzi huo, lakini muda ulikuwa umeenda sana na ilibidi niheshimu mkataba,” alieleza.

Jaribio la Kurudisha Pesa za Yanga Akiwa na shauku kubwa ya kurejea Msimbazi, Chama alichukua hatua ya kuwasiliana moja kwa moja na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, ili kuvunja mkataba huo.

“Nilimpigia simu Hersi na kumwambia: ‘Nitarejesha kila kitu mlichonipa, niambie mnahitaji nini ili nirudi Simba.’ Lakini aliniambia mashabiki na viongozi wote wa Yanga walikuwa tayari wananisubiri kwa hamu,” alisema.

Singida Black Stars Ilikuwa Njia ya Kubaki Karibu na Simba Baada ya kuitumikia Yanga na baadaye kujiunga na Singida Black Stars, Chama amefichua kuwa kuchagua Singida ilikuwa ni mbinu ya kimkakati ya kumfanya abaki karibu na Ligi Kuu ya Tanzania pamoja na Simba SC.

“Kama ningesaini timu ya Zambia, ningekuwa mbali sana na Simba. Singida ilikuwa ndiyo njia pekee ya kunifanya niwe karibu nao. Hata tulipokutana na viongozi wa Simba kwenye safari zetu, suala la mimi kurejea lilikuwa likijadiliwa,” aliongeza.

Ndoto Kutimia na Somo la Maisha Simba ilipompa nafasi ya kukaa na kusikiliza upande wake, Chama anasema ilikuwa ni kama maombi yake yamejibiwa.

Amehitimisha kwa kusema kuwa safari hiyo imemfundisha somo kubwa kwamba fedha na maslahi haviwezi kuleta furaha ikiwa mtu hana amani ya nafsi.

“Urafiki wangu na Watanzania ni mkubwa, hata wanangu wanajua kuimba wimbo wa taifa kwa Kiswahili. Nimejifunza kuwa unaweza kulipwa fedha nyingi sehemu fulani, lakini kama huna amani moyoni, inakuwa vigumu sana. Sasa hivi nimerejea Simba nikiwa na furaha, utulivu, na amani ya moyo.”

Milioni 3 Ziko Kwenye Meza Ya Fortune Frenzy Kukusubiri Steve Barker Tahadhari Mabedi: Simba SC Kuisambaratisha Mighty Wanderers Ligi ya Mabingwa