Sababu Kocha Mashujaa Akigoma Kumharakisha Jonas Mkude Uwanjani
Mashabiki wa soka nchini wanaosubiri kwa hamu kumuona kiungo mzoefu, Jonas Mkude, akirejea uwanjani watalazimika kuvuta subira kidogo. Hii ni baada ya Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Aman Josiah, kuweka wazi kuwa hana mpango wa kumharakisha mchezaji huyo.
Mkude, ambaye ana historia kubwa kwenye soka la Bongo akiwa amezichezea Simba SC na Yanga SC, alikaa nje ya uwanja kwa msimu mzima tangu alipoondoka kwa Wanajangwani msimu wa 2024/25, kabla ya kusajiliwa na Mashujaa FC kwa msimu wa 2026/27.
Akizungumza kuhusu hali ya kiungo huyo, Kocha Josiah alisisitiza kuwa kipaumbele chake ni kuhakikisha Mkude anarejea akiwa kwenye utimamu wa kutosha kimwili na kiakili, badala ya kuingia uwanjani kwa presha ya mashabiki.
“Hatuna sababu ya kumharakisha Mkude. Amekuwa nje kwa muda mrefu, kwa hiyo tunataka kumpa muda wa kutosha ili arudi vizuri. Tunataka kulinda hadhi yake na kuhakikisha akirudi anaweza kucheza katika kiwango ambacho watu wanamfahamu,” alisema Josiah.
Kocha huyo aliongeza kuwa Mkude anahitaji kujenga tena utimamu wa mwili, kasi ya mchezo pamoja na kujiamini kabla ya kutupwa kwenye ushindani wa mechi rasmi.
“Tunataka arudi akiwa tayari kabisa. Hatutaki acheze kwa sababu tu watu wanataka kumuona. Nataka siku atakaporejea iwe mwanzo wa sura mpya yenye kiwango bora, badala ya kurejea mapema kisha akashindwa kuonyesho uwezo wake,” aliongeza Kocha Josiah.
Mkude anasalia kuwa mmoja wa viungo wenye uzoefu mkubwa zaidi nchini, akitokea timu ya vijana ya Simba na kuitumikia timu ya wakubwa kwa zaidi ya miaka 12 kabla ya kutua Yanga. Uzoefu huo ndio unaofanya benchi la ufundi la Mashujaa FC kuwa makini zaidi katika mchakato wake wa kurejea uwanjani.