Tanzania U20 vs England U20
Michezo Bongo

Tanzania U20 vs England U20: Tanzanite Queens Kusaka Ushindi Wa Kihistoria Kombe La Dunia

Vardo September 8, 2026 11:02 am

Baada ya kuanza vibaya vibaya kwa kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya miamba ya soka Brazil, timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 20, Tanzanite Queens, leo inashuka tena kwenye Uwanja wa Stadion Miejski Bielsko-Biała nchini Poland saa 1:00 usiku kuwakabili England U20 katika mchezo wa pili wa Kundi B.

Kikosi hicho kinachofundishwa na kocha mzoefu Bakari Shime kina kibarua kizito dhidi ya England inayoshika nafasi ya tatu kwenye viwango vya ubora duniani vya FIFA, huku Tanzania ikiwa nafasi ya 122. Licha ya umbali mkubwa wa viwango, Tanzanite Queens inaingia uwanjani ikiwa na lengo moja tu: kupindua meza na kuandika historia mpya.

England Nayo Yatafuta Ushindi Wa Kwanza

England ilianza kampeni zake kwa sare ya 1-1 dhidi ya Canada, bao la kusawazisha likifungwa dakika ya 90 kwa penalti na Rachel Maltby. Matokeo hayo yanaifanya mechi ya leo kuwa ya vita kali, kwani ushindi wa timu yoyote utabadili kabisa msimamo wa Kundi B. Kwa Tanzania, kupata angalau pointi moja au ushindi utakuwa hatua kubwa kabla ya kukabili Canada kwenye mchezo wa mwisho wa kundi.

Mbinu 3 Tanzanite Queens Inazopaswa Kutumia Leo:

  1. Kupunguza Nafasi na Kuimarisha Ulinzi: Dhidi ya Brazil, safu ya ulinzi ilipata shida kwenye mipira ya pembeni na kasi ya katikati. Mabeki wanapaswa kuzuia mashambulizi mapema na kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu.

  2. Nidhamu ya Kiungo: Kiungo kinatakiwa kutulia na kutopoteza mipira kirahisi kwani England ina wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kubadilisha kasi ya mchezo.

  3. Kutumia Kasi ya Winfrida Gerald: Bao la mshambuliaji machachari Winfrida dhidi ya Brazil lilithibitisha kuwa Tanzania ina uwezo wa kufunga pindi inaposhambulia kwa ujasiri.

“Hii sio mwisho. Tutaendelea kupambana, michezo yetu bado ipo miwili. Tutaendelea kupambana michezo inayokuja tuweze kupata pointi. Kila mmoja atamsikiliza mwalimu na tutakuja kiukubwa kwenye mechi na England,” alisema Winfrida Gerald.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu ya soka ya wanawake ya Tanzania U20 kufuzu Fainali za Kombe la Dunia, na mechi ya leo ni fursa nyingine ya kudhihirisha kuwa kufuzu kwao nchini Poland hakukuwa kwa bahati mbaya.

Chipukizi Yaanza Vibaya Ligi Kuu Zanzibar: Mani Gamera Afunguka Sababu