Kocha Mwenge Msellem Sultan Hemed
Michezo Bongo

Msellem Sultan Hemed Aondoka Mwenge: Timu Mbili Za Pemba Zamwania

Vardo September 20, 2026 9:46 am

Aliyekuwa Kocha Mkuu wa klabu ya Mwenge FC, Msellem Sultan Hemed, amethibitisha rasmi kuachana na timu hiyo baada ya pande zote mbili kufikia makubaliano ya pamoja ya kusitisha mkataba wao.

Kujiondoa kwa kocha huyo kunakuja kufuatia mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar, ambapo Mwenge imepoteza mechi zote nne za mwanzo wa msimu huu. Katika michezo hiyo, Mwenge ilichapwa na Muembe Makumbi (2-0), Raskazone (2-1), Uhamiaji (2-0), na Black Sailors (2-1).

Akizungumza kuhusu uamuzi wake, Kocha Hemed alieleza kuwa mbali na matokeo mabaya, mazingira ya kazi hayakuwa rafiki kwa mpira wa kisasa.

“Ukiachana na sababu ya mfululizo wa matokeo mabaya kwa timu, sijaridhishwa na mazingira yake kwani sio ya mpira wa kisasa. Tumeachana kwa amani kabisa. Mpira una matokeo ya aina tatu, na nimeamua kupisha ili walimu wengine walete mbinu mpya zitakazoirejesha Mwenge kwenye ushindani,” alisema Hemed.

Timu Mpya Zaanza Mchakamchaka Wa Kumwania

Mara baada ya kutangaza kuondoka kwake, taarifa za ndani zinaeleza kuwa timu mbili kutoka Pemba zimeingia kwenye vita ya kuwania saini yake. Timu hizo ni:

  1. Wawi Stars – Inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

  2. Fufuni FC – Inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar.

Mwenyewe amethibitisha kuwa yupo kwenye mazungumzo na klabu nyingine kwa ajili ya kuchukua mikoba ya kufundisha hivi karibuni. Hemed anakuwa kocha wa pili kuondoka kwenye benchi la ufundi katika timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar msimu huu.

Lucas Kikoti Kujitafuta Namungo FC: Aweka Shabaha ya Mabao 10