Erik Mwijage Yanga
Yanga SC

Erik Mwijage Aanza Na Moto Yanga: Aweka Wazi Mipango Yake Na Ushindani Wa Namba!

Vardo September 20, 2026 8:39 am

KIUNGO mpya na machachari wa Yanga SC, Erik Mwijage, ameanza rasmi safari yake ya kupigania nafasi katika kikosi cha kwanza, baada ya kuonyesha cheche zake za kwanza tangu alipojiunga na mabingwa hao wa nchi katika dirisha kubwa la usajili.

Mwijage alipata fursa ya kukiwasha kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya miamba ya Ethiopia, St George, uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Mchezo huo ulikuwa kipimo muhimu kwake kuanza kuonja ladha na kasi ya ushindani ndani ya wananchi.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa pambano hilo, Mwijage hakusita kumshukuru Mungu pamoja na uongozi wa Yanga kwa kumpa fursa hiyo, huku akieleza kufurahishwa na mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki na wachezaji wenzake.

“Namshukuru Mungu kwa uwezo wake na pia nawashukuru wote walionipokea. Kwangu ni uzoefu maalumu na wa kipekee kukutana na mashabiki pamoja na wachezaji wenzangu wapya,” alisema Mwijage.

Kuhusu Vita Ya Namba Na Ushindani Ndani Ya Yanga

Akitambua ukubwa wa klabu hiyo na ubora wa wachezaji waliopo, kiungo huyo alikiri kuwa kuna ushindani mkubwa wa namba, lakini akathibitisha kuwa yuko tayari kwa mapambano hayo ili kuifanya Yanga izidi kutawala soka la Bongo.

“Yanga ina wachezaji wazuri sana na wanaofanya vizuri kwa sasa. Mimi kama mchezaji, nitazidi kujituma kama nilivyokuwa nikifanya huko nyuma. Kila nitakapopata nafasi kutoka kwa benchi la ufundi, nitahakikisha nafanya vizuri na kuonyesha kwanini nimesajiliwa hapa,” aliongeza.

Baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika dakika zake za kwanza uwanjani, mashabiki wa Yanga sasa wanasubiri kwa hamu kuona jinsi mchezaji huyo atakavyotumiwa kwenye mechi rasmi za ushindani, huku yeye akiwa amepania kutumia kila fursa kuthibitisha thamani yake.

Simo Dladla Afichua Eneo Yanga Inalotakiwa Kurekebisha Haraka Baada ya Kuichapa St George Simba Yaja na Mipango Mizito: Kuweka Kambi Afrika Kusini Kuisuka Kariakoo Derby