Rany Kida
Burudani

Kutoka Biharamulo Mpaka Jason Derulo: Historia na Mafanikio ya Dansa Rany Kida

Vardo September 25, 2026 10:23 am

Katika dunia ya burudani, kuna watu wanaofika kwenye kilele cha mafanikio kupitia majina makubwa ya wasanii. Hata hivyo, wapo wanaopambana kwa jasho na damu hadi kujenga utambulisho wao wenyewe bila kutegemea msaada wa mtu mwingine.

Miongoni mwao ni Rany Kida, dansa kijana aliyejijenga kwa umahiri mkubwa katika tasnia ya uchezaji (dance) nchini Tanzania na sasa anafanya kazi na wasanii mbalimbali wakubwa ndani na nje ya nchi.

Chimbuko la Jina ‘Rany Kida’

Safari yake inaanzia Biharamulo mkoani Kagera alipolelewa, ingawa asili yake ni Mnyakyusa. Jina lake halisi anaitwa Imran Said.

Akieleza chimbuko la jina lake la sanaa, Rany Kida anasema:

“Ran nimetengeneza kutoka kwenye jina langu la Imran (nimechukua sehemu ya mwisho). ‘Kida’ ina maana ya ‘King of Dance’, jina nililopewa baada ya kushinda mashindano ya uchezaji mwaka 2018. Kwa hiyo Rany Kida ni kama Ran King of Dance.”

Ushindi huo wa mwaka 2018 ndio uliokuwa mwanzo wa safari yake na kumpa utambulisho thabiti katika ulimwengu wa unenguaji.

Hakubebwa na Staa: Mapambano Dhidi ya Dhuluma na Kukataliwa

Tofauti na madansa wengi wanaopata umaarufu kupitia migongo ya wasanii wakubwa, Rany Kida alipita njia ya pekee yake. Njia hiyo haikuwa nyepesi kwani ilitawaliwa na changamoto za kukataliwa na kudhulumiwa maslahi yake.

“Nilipitia changamoto nyingi sana. Kuna wakati nilikataliwa na hata kudhulumiwa, lakini sikukata tamaa. Niliendelea kupambana mpaka nikajenga jina langu mwenyewe,” anasisitiza.

Leo hii, anafanya kazi na wasanii kulingana na mahitaji ya kazi zao. Kuhusu gharama za huduma zake, anafafanua kuwa hana bei moja ya kudumu: “Sina bei moja kwa kila msanii. Kuna msanii anayeanza na kuna msanii mkubwa, hivyo naangalia ukubwa wa kazi na mahitaji ya msanii mwenyewe.”

Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni kufanya kazi na staa wa kimataifa Jason Derulo, ambaye alimlipa fedha kwa ajili ya kushiriki kwenye video yake ya muziki.

Kulea Vipaji na Madarasa ya Dansi

Rany Kida haishii tu kwenye majukwaa na video za muziki, bali pia ni mwalimu anayeendesha madarasa ya mafunzo ya unenguaji:

  • Darasa la Jamii (Jumamosi): Mtu anachangia Sh5,000 pekee kushiriki.

  • Private Classes (Jumapili): Maalumu kwa wanaohitaji mafunzo binafsi kupitia miadi.

Kupitia madarasa haya, amefanikiwa kuinua vipaji vingi uchanga. Anaiambia jamii kuwa furaha yake kubwa ni kuona wanafunzi wake wanafanikiwa, kama vile mwanafunzi wake mmoja aliyepata fursa ya kufanya tangazo baada ya Rany kuunganisha familia ya mtoto huyo na mfanyabiashara.

Heshima na Thamani ya Madansa Nchini

Pamoja na hatua alizofikia, Rany Kida anaiomba jamii na sekta ya burudani kubadilisha mtazamo kuhusu madansa. Anasisitiza kuwa dansa ana mchango mkubwa wa kuufanya wimbo uitikike na usambae kwa kasi mitandaoni.

“Kuanzia kwenye malipo mpaka huduma tunazopata kwenye location, bado kuna changamoto. Mimi lazima niupende kwanza wimbo ndio niucheze au niufundishe. Siwezi kucheza wimbo kwa sababu tu nataka msanii anione,” anasema.

Nidhamu, Kipato na Maisha Binfasi

Kwa Rany Kida, uchezaji si hobby wala burudani ya pembeni—ni kazi rasmi inayomwingizia kipato cha kutosha.

  • 70% ya kipato chake kinatoka moja kwa moja kwenye sanaa ya dansi.

  • 30% inatoka kwenye biashara nyingine na fursa alizozipata kupitia mtandao wake wa kazi.

Kupitia kazi hii, ameweza pia kumhudumia mama yake mzazi. Pia anapinga mtazamo wa jamii kuwa madansa ni watu wa starehe na vilevi:

“Sijawahi kutumia kilevi cha aina yoyote. Ukiamua kufanya unenguaji kama kazi, unatakiwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu.”

Mambo 4 anayowashauri vijana ili kufanikiwa:

  1. Kuwa na nidhamu ya kazi.

  2. Kumtanguliza Mungu mbele.

  3. Kuzingatia muda.

  4. Kujiepusha kabisa na matumizi ya vilevi.

Ndoto ya Kuanzisha ‘Dance Academy’ Tanzania

Mbali na kucheza, kubuni mavazi, na kuimba, ndoto kubwa ya Rany Kida ni kuona taaluma ya dansi ikiingia kwenye mfumo rasmi wa elimu nchini.

“Nataka siku moja niwe na Dance Academy yangu. Nataka vijana wapate sehemu rasmi ya kujifunza kunengua kama taaluma na sio kucheza mitaani tu. Pia, ndoto yangu ndani ya miaka mitano ijayo ni kuona dance ya Tanzania inavuka mipaka na kuheshimika kimataifa.”

Siri Yafichuka! Kim Kardashian na Lewis Hamilton Wazama Kwenye Mapenzi Baada ya Miaka 12 Ngorongoro Heroes Yaangukia Pua Fainali CECAFA U20 Mbele ya Sudan