Arafat Ally
Habari za michezo

Arafat Ally Anasa Siri ya Soka la Misri, Aipiga Mkwara Bongo!

Vardo September 28, 2026 11:52 am

KIUNGO mshambuliaji wa Enppi SC inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri, Arafat Ally, ameweka wazi tofauti kubwa iliyopo kati ya mpira wa miguu wa Misri na Tanzania, akibainisha kuwa uwekezaji na mfumo thabiti wa kuendeleza vipaji vya vijana ndiyo nguzo kuu ya mafanikio yao.

Arafat, ambaye alikuwa nahodha na kinara aliyeiongoza Timu ya Taifa ya Vijana (U-20) kufuzu Fainali za AFCON U-20, ameeleza kuwa nchini Misri kuna ligi rasmi na maalum ya vijana. Mfumo huo umekuwa ukiwajenga wachezaji kisaikolojia na kimbinu tangu wakiwa wadogo kabla ya kupandishwa katika vikosi vya wakubwa.

Akifafanua zaidi, nyota huyo alisema kuwa klabu zote 20 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Misri zinalazimika kuwa na timu za vijana, jambo linalorahisisha mchakato wa kuandaa na kuibua nyota wapya wa baadaye.

“Ndiyo maana wenzetu wachezaji wengi ni rahisi kuuzika nje hata Ulaya, kwa sababu wana mfumo mzuri wa ligi ya vijana ambao unafuatiliwa kwa karibu sana,” alisema Arafat Ally.

Hata hivyo, kiungo huyo alionyesha matumaini na mwelekeo wa soka la Tanzania akisema:

“Hapa kwetu naona pia hilo limeanza kuonekana na naamini likiendelea, kuboreshwa zaidi na kusapotiwa kwa ukubwa, itakuwa moja ya ligi shindani sana za vijana.”

Huu ni msimu wa pili mfululizo kwa Arafat kuitumikia Enppi SC, baada ya kujiunga nayo msimu wa 2025/26 akitokea Namungo FC alipokuwa akicheza kwa mkopo kutoka Azam FC.

Vodacom Tanzania Yaungana Na Viongozi Wa Sekta Ya Biashara Katika Ceo Golf Tournament 2026 Sababu za Kipa Mpya wa Geita Gold, Kayode Bankole Kukosa Mechi za Ligi Kuu