Edwin Kagabo
Simba SC

Taarifa Njema Afya ya Kikosi cha Simba SC Afrika Kusini

Vardo September 30, 2026 6:29 pm

DAKTARI wa Simba SC, Edwin Kagabo, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo baada ya kutoa taarifa njema kuhusu hali ya afya ya kikosi kizima kilichopo nchini Afrika Kusini, akithibitisha kuwa hakuna mchezaji mwenye jeraha kubwa.

Simba hivi sasa ipo nchini Afrika Kusini ambako imeweka kambi maalum ya kujiandaa na kalenda nzito ya michezo iliyo mbele yao, ikizihusisha mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, Dabi ya Kariakoo dhidi ya watani zao Yanga SC, pamoja na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza kuhusu utimamu wa wachezaji, Dr. Kagabo ameeleza kuwa kikosi kipo kwenye hali nzuri na wachezaji wote wanaendelea na programu za mazoezi bila kikwazo chochote kikubwa.

“Kwa ujumla hali ya wachezaji ni nzuri sana. Wachezaji wote waliofika hapa Afrika Kusini wako kamili. Hata wale waliokuwa na changamoto za majeraha, ni matatizo madogo tu yanayotibika na hayajamzuia mchezaji yeyote kukaa nje kwa muda mrefu,” amesema Kagabo.

Daktari huyo ameongeza kuwa nidhamu ya afya na maandalizi mazuri yameisaidia Simba kuepuka majeraha ya muda mrefu tangu walipokuwa kwenye michezo ya ligi ya ndani na mashindano ya kimataifa.

Hali ya Wilson Nangu na Abdulrazack Hamza

Kuhusu wachezaji Wilson Nangu na Abdulrazack Hamza ambao wamekuwa wakisumbuliwa na majeraha hivi karibuni, Dr. Kagabo ameweka wazi kuwa wapo pamoja na timu nchini Afrika Kusini na wanaendelea vizuri na programu maalum kabla ya kurejea uwanjani kikamilifu.

“Wachezaji kama Nangu na Hamza tuko nao hapa Afrika Kusini. Wanaendelea vizuri na programu maalum ya mazoezi ya viungo (physiotherapy) ili kurejesha utimamu wao wa mwili kabla ya kuanza mazoezi ya pamoja na wenzao,” amehitimisha Kagabo.

Sakata la Israel Mwenda Yanga Chukua Sura Mpya, Akimbilia SPATA Meneja wa Simba Afunguka Sababu ya Kambi ya Afrika Kusini, Si Dabi Tu!