TRA United Benchi la Ufundi
Michezo Soka la Bongo

TRA United Yaivamia Yanga na Azam FC: Yanaswa Majina Mazito Benchi la Ufundi!

Vardo September 30, 2026 10:52 am

Klabu ya TRA United imeanza rasmi mchakato wa kusuka upya benchi lake la ufundi baada ya kuingia mikataba na wataalamu wenye uzoefu mkubwa kutoka klabu za vigogo, Yanga SC na Azam FC, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha kikosi hicho msimu huu.

Katika kuanza msimu, TRA United imepata matokeo ya kusuasua ambapo baada ya mechi sita (6) za Ligi Kuu, imeshinda mchezo mmoja tu, ikitoka sare mara tatu na kupoteza mechi mbili. Matokeo hayo yameiweka timu hiyo katika nafasi ya 12 kwenye msimamo ikiwa na pointi 6, huku ikifunga mabao sita na kuruhusu mabao sita.

Kutoka Azam FC na Yanga SC Mpaka TRA United

Baada ya kuimarisha baadhi ya maeneo kwa kuchukua wataalamu waliowahi kuhudumu Yanga, TRA United imeongeza nguvu nyingine kwa kumsajili Murshid Kika, aliyekuwa Kocha wa Mazoezi ya Viungo (Fitness Coach) wa Azam FC. Murshid amekabidhiwa jukumu la kuhakikisha utimamu wa mwili wa wachezaji unakuwa katika kiwango cha juu.

Mbali na Murshid Kika, TRA United ipo kwenye mazungumzo ya kina kumsajili mtaalamu wa uchambuzi wa mbinu na utendaji wa wachezaji (Performance & Tactical Analyst) wa Yanga, Bartalomew Prosper.

Mapendekezo ya Kocha Mpya Hemed Suleiman ‘Morocco’

Mchakato mzima wa kuleta wataalamu hawa unatokana na mapendekezo ya Kocha Mkuu mpya wa TRA United, Hemed Suleiman ‘Morocco’, ambaye anahitaji benchi la ufundi lenye ufanisi wa hali ya juu ili kutengeneza muunganiko imara wa kikosi.

Taarifa za ndani kutoka klabuni hapo zinaeleza:

“Tumekuwa tukisajili kutokana na mahitaji yetu na kuzingatia ubora wa wachezaji pamoja na nafasi ambazo tulihitaji kuzifanyia maboresho. Ndio maana tunaendelea kuongeza nguvu hasa kwenye eneo la ufundi ili mastaa wetu wazidi kunolewa na wataalamu wenye uzoefu.”

Ujio wa wataalamu hawa waliopitia timu zinazowania ubingwa nchini unaitengenezea TRA United msingi thabiti wa kushindana na kurejesha matokeo chanya kwenye michezo inayofuata ya Ligi Kuu.

Dabi ya Kariakoo: Mastaa wa Zamani Watabiri Vita Ngeni ya Makocha Simba na Yanga Kocha Coastal Union Afunguka Mipango Mizito ya Farid Mussa “Wakati Umefika”