Steve Barker Afunguka Kuhusu Doumbia Simba SC: “Atafunga Mabao Mengi”
Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amewasihi mashabiki na wadau wa soka waliokata tamaa na mshambuliaji Ibrahim Doumbia kuwa na subira, akisisitiza kuwa bado ana imani kubwa na raia huyo wa Mali.
Doumbia alijiunga na Wanalunyalunya akiwa miongoni mwa wachezaji waliotegemewa kubeba jukumu la ufungaji Msimbazi. Hata hivyo, hadi sasa hajafikia kiwango kinachotazamiwa kwenye ufungaji, jambo lililoibua maswali mengi miongoni mwa mashabiki.
Pamoja na kuanza kwa kusuasua, Kocha Barker ameweka wazi kuwa uwezo wa Doumbia haupaswi kupimwa kwa idadi ya mabao pekee kwa sasa. Amebainisha kuwa rekodi nzuri ya ufungaji aliyokuwa nayo kwenye timu yake ya zamani ndiyo sababu kuu inayomfanya aendelee kumwamini.
Barker ameeleza kuwa changamoto kubwa inayomkabili mshambuliaji huyo hivi sasa ni mchakato wa kuzoea timu mpya, mazingira ya nchi na mfumo mpya wa soka.
“Sidhani kama anahangaika kufunga Tanzania. Bahati mbaya anapitia mapito ya kawaida ya kuhamia timu mpya na ni suala la kiufundi tu. Muda si mrefu atafunga na sina shaka kabisa na hilo. Atafunga na atafunga mabao mengi mazuri,” alisema Barker.
Kwa sasa, Benchi la Ufundi la Simba SC linaendelea kumpa nafasi na utulivu Doumbia ili kuendana na mfumo wa timu, huku matumaini makubwa yakiwa ni kumuona anaanza kucheka na nyavu mara tu atakapokaa sawa.