Steve Barker Aivulia Vazi Yanga: “Dabi ya Kariakoo ni Vita ya Akili na Mbinu!”
Joto la Dabi ya Kariakoo kati ya Simba SC na Yanga SC limeanza kupanda kwa kasi kuelekea mchezo huo wa Oktoba 10. Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ametuma ujumbe mzito akieleza kuwa pambano hilo litakuwa vita ya mbinu na akili, ambapo kila upande utahitaji kusoma mipango ya mwenzake ili kutawala dakika 90.
Barker amebainisha kuwa Dabi hii itakuwa na utofauti mkubwa na michezo mingine kutokana na presha pamoja na ushindani mkubwa uliopo, akisisitiza kuwa matokeo yatategemea zaidi namna timu itakavyotumia makosa au mapungufu ya mpinzani wake.
“Watanzania wanaifuatilia kwa umakini mkubwa. Ni timu mbili zilizoanza ligi kwa rekodi nzuri sana. Itaenda kuwa mechi ya kipekee na ya kimbinu zaidi. Dabi ya Yanga ni vita ya utimamu wa mbinu na akili,” amesema Barker.
Kambi ya Afrika Kusini Yaijenga Simba SC
Akizungumzia maandalizi ya klabu hiyo nchini Afrika Kusini, Kocha Steve Barker ameeleza kuwa kambi hiyo imekuwa na manufaa makubwa mno kwa kikosi chake ukilinganisha na maandalizi waliyofanya kabla ya mchezo wa Ngao ya Jamii.
Simba SC tayari imeshinda michezo sita mfululizo, na Barker amethibitisha kuwa na shauku kubwa ya kuendeleza mfululizo huo wa ushindi kwenye mechi ya dabi.
-
Maandalizi: Yamefikia kiwango cha juu kuliko mwanzo wa msimu.
-
Lengo: Kusaka ushindi wa saba mfululizo kwenye Ligi Kuu.
Presha ya Ukocha na Wito kwa Mashabiki
Kuhusu presha ya benchi la ufundi, Barker amesema presha ni sehemu ya maisha ya ukocha, lakini kwake yeye presha kubwa inatoka kwenye hamu ya kutaka kuleta mafanikio makubwa ndani ya Simba SC na si hofu ya mpinzani.
Pia ametoa wito mzito kwa mashabiki wa Msimbazi kujitokeza kwa wingi uwanjani siku ya mchezo ili kuwa mchezaji wa 12:
“Ni mechi yetu ya nyumbani, tunawahitaji mashabiki kuwa nyuma yetu kwa asilimia 100. Tunawaomba waishikilie timu yao na wajitokeze kwa wingi kututia moyo.”
Changamoto ya Kuwa Mbali na Familia
Mbali na masuala ya uwanjani, Barker ameweka wazi changamoto za kibinafsi anazopitia kwa kuwa mbali na familia yake iliyopo Afrika Kusini. Ameeza kuwa mwanaye amemaliza shule na anaishi na mama yake, lakini anawasiliana nao kila siku kwa njia ya simu na video.
Licha ya changamoto hiyo, Barker amesisitiza kuwa ana mpango wa kukaa Simba SC kwa muda mrefu na siku zijazo ataungana na familia yake hapa nchini, huku mapumziko ya kalenda ya FIFA yakimpa nafasi ya kwenda kuwasalimia.