Fainali ya Ligi ya Viziwi Zanzibar: Hope Deaf City Kukipiga na Wakombozi Kesho
FAINALI ya Ligi ya Viziwi Zanzibar kati ya timu ya Hope Deaf City na Wakombozi inatarajiwa kuchezwa kesho Jumamosi jioni, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein.
Taarifa hiyo imetolewa leo Oktoba 2, 2026 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Michezo ya Viziwi Zanzibar (SHIMIVIZA).
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa ZFF, Namala Suleiman, amesema mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kati ya Zan Deaf na Vuka City utaanza majira ya saa 8:00 mchana, kabla ya kuchezwa kwa mechi ya Fainali saa 10:00 jioni.
“Fainali ya Ligi ya Viziwi itachezwa kesho, hivyo tunawaomba mashabiki wafike uwanjani kwa wingi kuwapa hamasa wachezaji wetu kama ilivyo kwenye mechi nyingine,” amesema Namala.
Amefafanua kuwa ligi hiyo ni miongoni mwa mipango madhubuti ya ZFF katika kuendeleza na kusimamia soka la watu wenye ulemavu Zanzibar.
Kwa upande wake, Katibu wa SHIMIVIZA, AbdulAzizi Mohammed Mahfoudh, amelishukuru shirikisho la ZFF kwa kukubali kuwaunga mkono na kuwapa fursa wachezaji wenye ulemavu wa kusikia kuonyesha vipaji vyao.
AbdulAzizi ameeleza kuwa baada ya mashindano haya ya kwanza yaliyoshirikisha timu nne kufanikiwa, tayari zimejitokeza timu 12 zinazotaka kushiriki ligi inayofuata ili kupata wachezaji watakaoiwakilisha Zanzibar katika mashindano ya kimataifa.
Amehitimisha kwa kusema kuwa wapo wachezaji wengi viziwi wenye vipaji vikubwa ambao walikuwa hawajapata jukwaa la kuvionyesha, na kuanzishwa kwa ligi hii kutoa fursa mpya kwa jamii kufurahia viwango vyao uwanjani.