Mbwana Samatta akiwa na jezi ya Le Havre mwaka 2026
Life Style

Maisha Ya Mbwana Samatta Nje Ya Uwanja: Utajiri Wa Bilioni 20–30, Magari, Hekalu Kigamboni Na Skendo Zake

admin October 3, 2026 8:33 am

Kuna wachezaji wamecheza Ulaya, kuna waliopiga pesa Ulaya, halafu kuna Mbwana Ally Samatta.

Safari yake ilianza kwenye maisha ya kawaida kabisa, hadi kufikia wakati African Lyon ilipoanza kumlipa mshahara wa karibu TSh 140,000 kwa mwezi — wakati huo ikiwa sawa na takribani Pauni 40.

Kutoka hapo akavaa jezi ya Simba SC, kisha TP Mazembe, Genk, Aston Villa, Fenerbahce, Royal Antwerp, akarudi Genk, akapita PAOK na sasa anakipiga Le Havre ya Ligue 1.

Na miaka yote hiyo haijapita bure.

Samatta ambaye sasa ni staa wa zamani wa Taifa Stars baada ya kutangaza kustaafu soka la kimataifa Julai 2026, amejenga CV ambayo kwa mchezaji wa Kitanzania si ya kawaida kabisa.

Mafanikio Ndani Ya Uwanja

Kabla hata hujafungua pochi yake, CV yake yenyewe inatosha kueleza huyu jamaa alifika level gani.

TimuMechi Za LigiMabao Ya LigiKilichobaki Kwenye Historia
Simba SC2513Aling’ara haraka na hata kwenye CAF akafunga; ndipo TP Mazembe wakamnasa
TP Mazembe10360Mabingwa wa CAF Champions League 2015, mataji manne ya ligi DR Congo, Super Cups mbili
KRC Genk17762Bingwa Ubelgiji 2018/19, Belgian Super Cup, mfungaji bora wa ligi na Ebony Shoe
Aston Villa141Mtanzania wa kwanza kucheza na kufunga Premier League; alifunga pia fainali ya Carabao Cup
Fenerbahce305Moja ya mikataba yake mikubwa zaidi kifedha
Royal Antwerp325Alirudi tena Ubelgiji kwa mkopo
PAOK416Bingwa wa Super League Greece 2023/24
Le Havre32+5+Bado yupo Ligue 1; msimu wa 2026/27 alianza kwa mabao mawili ndani ya mechi tano
Taifa Stars8722Nahodha wa muda mrefu, AFCON mara tatu kabla ya kustaafu 2026

Na Afrika Cup of Nations yenyewe Samatta hakuishia kuiona kwenye TV.

Alicheza AFCON 2019, akatokea tena AFCON 2023, kisha akacheza AFCON 2025 kabla ya kutundika jezi ya Taifa Stars. Katika fainali hizo tatu pekee alifikisha jumla ya mechi 10, huku bao lake la AFCON likija mwaka 2019.

Kwenye TP Mazembe ndipo CV iliponenepa zaidi. Samatta akawa Mfungaji Bora wa CAF Champions League 2015, akatwaa Champions League yenyewe na baadaye akachaguliwa Mchezaji Bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani ya bara.

Ubelgiji nako akachukua ligi na Genk, akawa mfungaji bora na akabeba Ebony Shoe.

PAOK akachukua ubingwa Ugiriki.

Hiyo ndiyo CV iliyotengeneza pesa tunazozizungumza hapa chini.

Utajiri Wake: TSh Bilioni 20 Hadi 30

Mbwana Samatta anakadiriwa kuwa na utajiri wa kati ya TSh bilioni 20 hadi 30 kwa sasa.

Humo kuna nyumba, magari, miradi, fedha na mali nyingine alizojenga katika zaidi ya miaka 15 ya kucheza soka la kulipwa.

Lakini kupata picha ya namna mzigo huo ulivyotengenezwa, lazima urudi kwenye mikataba yake.

Takwimu za mishahara ya career yake Ulaya zinaonyesha ameshavuta makumi ya mabilioni kwa mishahara pekee. Ukiongeza signing bonuses, performance bonuses na mapato ya mikataba mingine, Samatta anakadiriwa kuwa ameshaingiza zaidi ya TSh bilioni 45 hadi 50 katika career yake yote.

Hapo ndiyo tofauti ilipo.

TSh bilioni 45–50 ni makadirio ya fedha ambazo career yake imezalisha kwa miaka yote; TSh bilioni 20–30 ndiyo makadirio ya utajiri wake wa sasa baada ya kodi, matumizi, uwekezaji na mali alizokusanya.

Signing Fees: Kila Akiweka Sahihi, Kibunda Kinaingia

Samatta hakutengeneza hela kwa mshahara pekee.

Kwenye mikataba mikubwa, wachezaji hupokea signing bonuses na incentives kulingana na hadhi yao na mazingira ya dili.

Lakini kabla ya mabilioni ya Mazembe na Ulaya, kulikuwa na Simba SC — na hapa kulikuwa na kasakata lake.

Simba, Gari Na Mgomo Wa Samatta

Simba ilimsajili Samatta kutoka African Lyon mwaka 2010 kwa mkataba uliokuwa wa miaka miwili, lakini kijana huyo hakukubali mambo yaende tu kwa sababu alikuwa amepewa jezi nyekundu.

Kulikuwa na madai ya fedha zake za usajili ambazo zilikuwa hazijakamilishwa pamoja na gari aliloahidiwa wakati wa kusaini.

Samatta akakaza.

Akasusa.

Akagoma kuripoti na kucheza hadi Simba wakamilishe walichokuwa wamemuahidi.

Hiyo ilikuwa kabla hajawa Samatta wa mabilioni, lakini tayari kichwani alikuwa ameshaelewa kitu kimoja — mkataba ni mkataba.

Baada ya madai yake kutatuliwa akarudi kikosini na hapo ndipo akawasha moto.

Mwaka mmoja tu Simba ukatosha kuwafanya TP Mazembe waone kuna kitu hapa. Kwenye CAF akakutana nao, akafanya yake na safari ya kwenda DR Congo ikaanza.

Hapo ndipo maisha yakaanza kubadilika kweli.

Akienda TP Mazembe mwaka 2011, Samatta alikuwa bado anapandisha jina lake lakini tayari alikuwa ameshaanza kuvutia timu nje ya Tanzania.

Signing package yake Mazembe inaweza kukadiriwa kuwa karibu TSh milioni 150 hadi 300.

Alipohamia Genk mwaka 2016, alikuwa tayari ametoka kuwa Mchezaji Bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani ya bara na mshindi wa CAF Champions League.

Hapa mezani hapakuwa tena na hela ndogo.

Signing package yake Genk inaweza kukadiriwa kati ya TSh milioni 600 hadi zaidi ya bilioni moja.

Mwaka 2020 ndiyo mlango mkubwa ukafunguka — Aston Villa.

Villa walimchukua kutoka Genk kwa dili lililoripotiwa kufikia karibu Pauni milioni 8.5–10. Hiyo ilikuwa transfer fee ya klabu kwa klabu, lakini Samatta mwenyewe pia alikuwa na mkataba wake.

Kwa mazingira ya Premier League na mkataba wa miaka minne na nusu, signing package yake inaweza kukadiriwa kwenye TSh bilioni 1 hadi 2.

Fenerbahce nayo ikamchukua mwaka huo huo. Dili la Uturuki lilikuwa na mshahara mzito na mazingira yake yanaweka signing package inayoweza kukadiriwa kwenye TSh bilioni 1 hadi 2.

Royal Antwerp, kurejea Genk, PAOK na sasa Le Havre nazo zilikuwa na packages tofauti.

Kwa ujumla, signing bonuses na loyalty packages katika career yake yote zinaweza kuwa zimemwingizia takribani TSh bilioni 4 hadi 7.

Mishahara: Hapa Ndipo Mabilioni Yalipotengenezwa

Genk ndiyo iliyoanza kumfungulia bomba la Ulaya.

Katika misimu yake ya mwanzo Ubelgiji, mshahara wake ulikadiriwa karibu TSh milioni 592 kwa mwaka, sawa na takribani Euro 200,000 kwa thamani ya sasa ya fedha.

Kadri mabao yalivyoingia, mshahara ukapanda.

Kufikia moja ya misimu yake mikubwa Genk, Samatta alikadiriwa kufikia karibu TSh bilioni 2 kwa mwaka, sawa na takribani Euro 690,000.

Kisha Aston Villa ikaja.

Premier League ikampeleka kwenye daraja jingine kabisa la mshahara. Samatta alikadiriwa kuwa kwenye karibu TSh milioni 139 kwa wiki, sawa na takribani Pauni 40,000.

Ndiyo — karibu TSh milioni 140 kila baada ya siku saba.

Halafu akaenda Fenerbahce ambako package yake ilifikia kiwango kinachokadiriwa kuwa zaidi ya TSh bilioni 10 kwa mwaka kwa thamani ya sasa ya fedha.

Huo ndio ulikuwa mmoja wa mikataba mizito zaidi kuwahi kushikwa na mwanasoka wa Tanzania.

Vipindi vya Royal Antwerp, Genk na baadaye PAOK navyo viliendelea kumpa mishahara ya kiwango cha juu Ulaya.

Mshahara Wake Ufaransa

Samatta sasa yupo Le Havre ya Ligue 1.

Mshahara wake wa msingi wa msimu wa 2026/27 unakadiriwa kuwa karibu TSh bilioni 3.2 kwa mwaka, huku package yenye bonuses ikiweza kufika karibu TSh bilioni 4.

Kwa mwaka: karibu TSh bilioni 3.2–4
Kwa mwezi: karibu TSh milioni 270–335
Kwa wiki: karibu TSh milioni 62–77

Yaani wiki moja ya Samatta inaweza kuwa mshahara wa miaka kadhaa kwa Mtanzania mwingine.

Kibunda Alichovuna Career

Ukichukua mishahara yake TP Mazembe, Genk, Aston Villa, Fenerbahce, Antwerp, PAOK na Le Havre, ukaweka signing packages na bonuses pembeni yake, career ya Samatta inaweza kuwa imeshaingiza zaidi ya TSh bilioni 45 hadi 50.

Ndiyo msingi mkubwa unaofanya utajiri wake wa sasa kukadiriwa kati ya TSh bilioni 20 na 30.

Magari: Range Rover Ya Zaidi Ya TSh Milioni 200

Edo Kumwembe alipokwenda kufanya mahojiano naye Ubelgiji, Samatta hakuficha sana maisha yake upande wa magari.

Moja ya mashine zake ilikuwa Range Rover aliyosema aliinunua cash.

Bei yake ilikuwa karibu Euro 68,000 — kwa thamani ya sasa ni zaidi ya TSh milioni 200.

Na hakuchukua loan.

Cash.

Mbwana Samatta akiwa juu ya Range Rover yake nchini Ubelgiji

Kabla yake alikuwa pia na Chrysler aliyokuwa akiitumia wakati wa TP Mazembe na baadaye gari hilo likaletwa Tanzania.

Kwa miaka tofauti ameonekana pia kwenye mashine za kiwango cha Land Cruiser, Prado na Mercedes-Benz, hasa anapokuwa Tanzania.

Lakini Range Rover na Chrysler ndiyo ambazo historia yake ya umiliki imewahi kuwekwa wazi zaidi.

Samatta si wale mastaa wa kupaki magari matano mstari mmoja halafu kupiga picha Instagram, lakini mashine amepita nazo.

Majumba: Kibada Alibomoa Jumba La Milioni 500, Akaanza Upya

Hapa ndiyo Samatta ana story nyingine.

Akiwa bado TP Mazembe alianza kujenga nyumba kubwa Kibada, Kigamboni.

Jengo likafika mbali.

Fedha karibu TSh milioni 500 zikawa tayari zimeingia.

Samatta akalitazama.

Hakupendezwa.

Akalibomoa.

Akaanza upya.

Jengo jipya lilivyoendelea, gharama zikavuka TSh bilioni moja, huku ripoti nyingine zikifika hadi karibu TSh bilioni 1.8.

Huko ndiko kukaja kuwa moja ya majumba yanayotambulika zaidi yanayohusishwa na mwanasoka huyo.

Jumba la Mbwana Samatta lililopo Kibada Kigamboni

Ndani yake kumewahi kuripotiwa kuwa na swimming pool, gym, bustani, parking kubwa, eneo la barbecue, kaunta na sehemu ya kuchezea mpira.

Na Kibada si mali pekee iliyowahi kutajwa.

Majina ya maeneo kama Majimatitu, Mbande, Mbagala Saku na Kiburugwa/Shimo la Mchanga yamewahi kuonekana kwenye simulizi za mali na uwekezaji wake wa nyumba.

Kwa mtu aliyekuwa akikusanya mabilioni Ulaya, sehemu kubwa ya hela ikaingia kwenye ardhi na majengo.

Biashara: Tours, SamaPay Na Foundation

Mpira unaweza kuisha. Samatta hilo aliliona mapema.

Aliwahi kuanzisha shughuli za utalii kupitia Mbwana Samatta Tours and Safaris, biashara iliyokuwa na mpango wa kufanya shughuli Dar es Salaam na Arusha.

Gari aina ya Alphard lilikuwa limetajwa kuwa moja ya magari yaliyotayarishwa kwa shughuli hiyo.

Kisha likaja jina la SamaPay, app ya malipo iliyohusishwa na Samatta na ambayo iliwahi hata kuingia kwenye mijadala mikubwa ya watumiaji mtandaoni.

Leo hii pia kuna Samatta Foundation, inayojikita kwenye michezo, elimu, afya na kusaidia jamii.

Na kule Vikindu, Mkuranga, Samatta alijenga msikiti mkubwa wenye uwezo wa kuchukua mamia ya waumini.

Hayo ndiyo maisha yake mengine ambayo hayapati headlines nyingi kama mabao.

Soma Hapa: Maisha Ya Clement Mzize Nje Ya Uwanja: Duka, Hisa Na Mabilioni Ya Dili

Mke, Watoto Na Familia

Upande wa nyumbani, Samatta amekuwa mchoyo wa habari.

Ana mke wake Naima, ambaye alifunga naye ndoa katika sherehe iliyofanyika kwa usiri mkubwa.

Hata media hazikutakiwa kugeuza harusi hiyo tamasha.

Mbwana Samatta akiwa na mke wake Naima katika picha ya harusi

Wawili hao wamewahi kuripotiwa kuwa na watoto wawili, Karim na Isimini.

Na kama kuna mtu mwingine ambaye alikuwa karibu sana na safari ya Samatta, basi ni baba yake, marehemu Mzee Ally Pazi Samatta.

Mzee Samatta alikuwa mmoja wa watu wachache walioweza kusimulia mambo ya mwanawe ambayo Samatta mwenyewe asingekaa kuyasema kwenye camera.

Mbwana Samatta akiwa na baba yake marehemu Ally Pazi Samatta

Alizungumza kuhusu nyumba zake, magari, biashara, safari ya mpira na hata mambo ya familia.

Kifo chake kilimuondolea Samatta mtu ambaye alikuwa zaidi ya baba — alikuwa mmoja wa mashabiki na washauri wake wakubwa.

Skendo? Hapa Kumkamata Samatta Ni Kazi

Kupata superstar wa level ya Samatta ambaye ana folder nyembamba kiasi hiki la skendo si kawaida.

Sababu?

Jamaa hayupo sana kwenye parties, vijiwe vya starehe, matamasha na kamera za showbiz.

Anaweza kutua Dar es Salaam, akaingia nyumbani, akaonekana kwa watu wake wachache na akarudi Ulaya bila hata nusu ya mjini kujua alikuwa hapa.

Irene Uwoya

Moja ya story zilizowahi kuchangamka sana ilihusisha jina la Irene Uwoya.

Mwaka 2016, baada ya Samatta kutwaa tuzo kubwa ya CAF, mijadala ya mitandaoni ilianza kumhusisha na mastaa mbalimbali wa Bongo Movie, huku Uwoya akiwa miongoni mwa majina yaliyotajwa.

Ndipo zikazaliwa simulizi kwamba kulikuwa na ukaribu uliotaka kugeuzwa kuwa headline kubwa zaidi ya ulivyokuwa.

Kuna story iliyozunguka kwamba waandishi walitaka kumnasa akiwa Serena, lakini Samatta aliposhtukia mazingira hayo akaondoka chap.

Samatta mwenyewe hakuwahi kuthibitisha mahusiano na Uwoya, na story hiyo ikaishia kubaki moja ya udaku uliopita sana mjini wakati huo.

Akagomea Dili, Akatibuana Na Wakala

Kulikuwa pia na wakati dili la kwenda Dinamo lilipoleta msuguano.

Samatta alikataa mpango huo licha ya presha iliyokuwepo, jambo lililoelezwa kuwa liliweka uhusiano wake na wakala kwenye hali mbaya.

Hiyo haikuwa skendo ya mapenzi, lakini ilikuwa moja ya drama kubwa za nyuma ya pazia katika career yake.

SamaPay Ikaja Na Maswali

SamaPay nayo haikupita bila kelele.

Baadhi ya watumiaji walipoanza kuitumia waliibua malalamiko kuhusu mfumo wa usajili, verification na experience ya app.

Jina la Samatta likawa linajadiliwa tena — safari hii si kwa goli wala transfer, bali biashara.

Lakini ukilinganisha na miaka yote ambayo amekuwa celebrity mkubwa Tanzania, hiyo ni rekodi safi sana.

Ana mabilioni.

Ana magari.

Ana nyumba.

Ana familia.

Amecheza Premier League.

Amezunguka ligi kubwa Ulaya.

Amevaa jezi ya Taifa Stars mara 87, akafunga mabao 22, akawa nahodha kwa miaka mingi halafu akaondoka kwa heshima yake.

Lakini kupata picha ya Samatta anatoka club saa kumi alfajiri na ugomvi pembeni?

Hapo ndipo utasubiri sana.

Fainali ya Ligi ya Viziwi Zanzibar: Hope Deaf City Kukipiga na Wakombozi Kesho