Bernard Kamungo Taifa Stars
Taifa Stars

Sababu za Bernard Kamungo Kuondoka Kambini Taifa Stars na Kurejea Marekani

Vardo October 2, 2026 9:40 am

Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Bernard Kamungo, ametatua rasmi changamoto ya nyaraka zake za usafiri na kuondoka kambini Morocco kurejea Marekani kujiunga na klabu yake ya FC Dallas.

Taarifa kutoka ndani ya kambi ya Taifa Stars zinaeleza kuwa nyota huyo amekamilisha taratibu zote za kupata hati yake ya kusafiria (passport) ya Tanzania kabla ya kufanya safari hiyo.

Hatua hiyo inamfanya Kamungo kukosa mechi za kirafiki za kimataifa zinazoendelea hivi sasa chini ya kalenda ya FIFA, kutokana na kuitwa kwa dharura na klabu yake inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani (MLS).

Kwanini FC Dallas Imemwita kwa Haraka?

Klabu ya FC Dallas inamhitaji mshambuliaji huyo kwa ajili ya mechi muhimu za ligi kuu zinazoendelea nchini Marekani. Kutokana na ratiba hiyo kubana, uongozi wa timu hiyo uliomba mchezaji huyo arejee klabuni mara baada ya kukamilisha taratibu zake za uraia na pasipoti.

“Ni kweli Kamungo amepata passport yake na tayari ameondoka kambini kuelekea Marekani. FC Dallas wamemhitaji kwa haraka sana kwa ajili ya mechi zao za ligi kuu,” kilieleza chanzo hicho cha ndani.

Lini Kamungo Atarejea Taifa Stars?

Mashabiki wa Taifa Stars watasubiri hadi mwezi Novemba 2026 kumuona tena Kamungo akiwa kikosini, wakati timu hiyo itakapokuwa ikikabiliwa na mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Kuondoka kwa Kamungo kunahitimisha sitofahamu iliyokuwepo kuhusu nyaraka zake za uraia tangu alipowasili kikosini chini ya Kocha Miguel Gamondi. Ingawa alijumuishwa kwenye kikosi kilichoandaliwa kuvaana na Guinea Bissau pamoja na Madagascar, hakuweza kucheza mechi hizo kutokana na kukwama kwa taratibu hizo za kisheria.

Kuhusu Bernard Kamungo

Kamungo, ambaye alizaliwa nchini DR Congo na kukulia katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma, Tanzania, alianza safari yake ya soka la kulipwa nchini Marekani. Alipata umaarufu mkubwa alipokuwa akiichezea klabu ya North Texas (2021–2022) kwenye Ligi Daraja la Tatu, ambapo alifunga mabao 22 katika mechi 52 kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza cha FC Dallas.

Steve Barker Aivulia Vazi Yanga: “Dabi ya Kariakoo ni Vita ya Akili na Mbinu!” Ally Salum Aanza Mazoezi Kagera Sugar, Aahidi Makubwa Ligi Kuu