Pacome Zouzoua
Yanga SC

Pacome Zouzoua Aweka Magongo Chini Yanga SC: Aanza Mchakato wa Tiba Nje ya Nchi

Vardo October 2, 2026 5:27 pm

Kiungo mshambuliaji wa Yanga SC, Pacome Zouzoua, amepiga hatua nyingine kubwa katika mchakato wa kuuguza jeraha lake la kifundo cha mguu baada ya rasmi kuacha kutembea kwa kutumia msaada wa magongo.

Pacome alipata jeraha hilo baya kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara msimu uliopita dhidi ya JKT Tanzania, jeraha ambalo linatarajiwa kumweka nje ya uwanja kwa msimu mzima.

Hatua kwa Hatua ya Uponaji wa Pacome

Baada ya kufanyiwa upasuaji wa awali na kuondolewa chuma kilichowekwa kwenye jeraha lake, nyota huyo raia wa Ivory Coast sasa ana uwezo wa kutembea mwenyewe bila msaada wa magongo mawili aliyokuwa akiyatumia hapo awali.

Inakumbukwa kuwa Septemba 10, 2026, Pacome alifika katika uwanja wa mazoezi wa Yanga akiwa bado anatumia magongo kuwashuhudia wenzake wakijiandaa na mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Gaborone United.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, kiungo huyo alionekana tena mazoezini akiwa ametupa magongo hayo na kutembea taratibu. Ingawa bado anachechemea kwa mbali, tabasamu kubwa usoni mwake lilidhihirisha furaha aliyonayo kwa hatua hiyo.

“Ni hatua kubwa sana naendelea kuipiga. Namshukuru Mungu naendelea vizuri, na nimefurahi tena kugusa nyasi za uwanja huu nikitembea kwa miguu yangu mwenyewe,” alisema Pacome akiwa na furaha tele.

Safari ya Matibabu Nje ya Nchi

Pamoja na hatua hiyo nzuri, taarifa kutoka ndani ya jopo la madaktari wa Yanga SC zinasema kuwa mchezaji huyo bado ana safari ndefu kabla ya kurejea uwanjani kikamilifu.

Daktari kutoka jopo la matibabu la timu hiyo alieleza:

“Hatua anayopiga mpaka sasa ni kubwa na anapona vizuri. Kufika hapa ni jambo la kumshukuru Mungu, lakini bado ana safari kidogo ya kuwa sawa kabisa. Tunatarajia wakati wowote kuanzia sasa ataanza hatua nyingine ya matibabu zaidi ambayo inaweza kufanyika nje ya nchi.”

Mashabiki wa Wananchi wanaendelea kumuombea kiungo huyo mahiri ili aweze kurejea kwenye hali yake ya kawaida na kuanza tena kutoa burudani uwanjani.

Maajabu Ya Orodha Ya Timu 10 Zenye Mashambulizi Makali Ulaya: Real Madrid Yaangukia Pua, Brighton Yaweka Rekodi Zanzibar Spice Boys Kwenda Brazil: Tazama Ratiba na Kundi Lao PQ CUP 2026!