De Reuk Aipigia Yanga Mkwara Mzito: “Tuko Tayari Kwa Dabi ya Kariakoo!”
Nahodha wa Simba SC, Rushein De Reuk, ameibuka na ujumbe mzito baada ya kumalizika kwa kambi ya siku 10 nchini Afrika Kusini, akisisitiza kuwa Wekundu wa Msimbazi wamerejea wakiwa na nguvu, umoja na kujiamini zaidi, huku macho yao yakiwa yameelekezwa kikamilifu kwenye Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga SC.
De Reuk ameeleza kuwa kambi hiyo imekuwa sehemu muhimu kwa kikosi chao kuendeleza kazi nzuri iliyoanza mwanzo wa msimu, huku wakitumia muda huo kuongeza ubora, kujenga mshikamano na kujiandaa na ratiba ngumu inayowasubiri mwezi huu.
Licha ya Simba kuanza msimu kwa kiwango kizuri, nahodha huyo amebainisha kuwa bado kuna maeneo yanayohitaji maboresho ili timu hiyo iwe bora zaidi.
“Msimu ulivyoanza hadi sasa, tumekuwa tukifanya vizuri, lakini tunafahamu bado kuna maeneo mengi ambayo tunahitaji kuboresha. Kambi hii imetupa nafasi ya kuendeleza kile ambacho tumekuwa tukikifanya na kuongeza ubora zaidi. Kwa ujumla ni jambo zuri,” amesema De Reuk.
Afurihia Michezo ya Kirafiki na Kuwasifu Makinda
De Reuk pia ameeleza kuridhishwa na michezo miwili ya kirafiki waliyocheza nchini Afrika Kusini, akisema ilikuwa kipimo kizuri cha kuangalia kiwango cha kikosi na kubaini maeneo yanayohitaji marekebisho.
Nahodha huyo mwenye uzoefu wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) alisema wapinzani waliokutana nao hawakuwa wepesi, lakini mechi hizo zimewapa taswira nzuri kuelekea hatua inayofuata ya maandalizi.
Aidha, aliwapongeza baadhi ya wachezaji makinda walipata nafasi ya kuonyesha uwezo wao—akiwataja Nindi, Nashon, na Bashir—kwa namna walivyopambana na kutoa mchango mkubwa kikosini.
Dabi ya Kariakoo: Yanga Kupimwa Nguvu!
Akizungumzia Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga, De Reuk amesema wanafahamu vyema ukubwa wa mchezo huo na presha yake, lakini ana imani kubwa kuwa maandalizi ya Afrika Kusini yamewapa silaha zote za kukabiliana na changamoto hiyo.
“Ni dabi, tena dhidi ya Yanga, hivyo si timu rahisi kucheza nayo. Lakini ninaamini katika kundi tulilonalo na ninaamini tunaweza kufanikisha jambo kubwa na la kipekee msimu huu,” aliongeza nahodha huyo.
Amwaga Sifa Kibao kwa Mo Dewji
Katika hatua nyingine, De Reuk amemshukuru Rais wa Heshima wa Simba, Mo Dewji, kwa uwekezaji na ushirikiano wake kwa klabu hiyo, akisema wachezaji wanatambua juhudi zake za kuhakikisha timu inapata mazingira bora.
Amesisitiza kuwa jukumu la wachezaji hivi sasa ni kupambana uwanjani na kumrudishia shukrani kwa kuleta matokeo chanya.
“Tunamshukuru sana kwa kila kitu anachofanya na kwa namna anavyotuunga mkono. Njia pekee tuliyonayo ya kumlipa ni kuhakikisha tunafanya vizuri na kutoa kiwango bora kila wiki. Kwa niaba ya wachezaji, ningenda kumshukuru kwa kila kitu,” alisema.
De Reuk alitimisha kwa kusema kuwa tangu atue Simba amekuwa akifurahia mazingira ya klabu hiyo na kwamba kuvaa jezi ya Wekundu wa Msimbazi ni dhamana kubwa kutokana na ukubwa wa klabu na matarajio ya mashabiki.