Simba SC Dabi ya Kariakoo
Simba SC

Simba SC Kutua Dar Leo na Ujumbe Mzito: Dabi ya Kariakoo Ndio Kila Kitu!

Vardo October 4, 2026 9:44 am

Dar es Salaam. Baada ya kukamilisha siku 10 za kambi ya maandalizi nchini Afrika Kusini, miamba ya soka nchini, Simba SC, imetua nyumbani ikiwa na ujumbe mzito kutoka kwa Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, kuelekea mchezo wao wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, utakaochezwa Oktoba 10.

Rweyemamu amebainisha kuwa kambi hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kukamilisha mipango yote iliyowekwa na benchi la ufundi chini ya Kocha Steve Barker, huku akisisitiza kuwa sasa akili na nguvu zote zimeelekezwa kwenye pambano hilo lililobeba hisia za mashabiki wengi.

Simba iliyondoka nchini Septemba 24 na kurejea leo Jumapili, inaingia moja kwa moja kwenye maandalizi ya mwisho kabla ya kuwakabili wanalambalamba na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu.

Manufaa ya Kambi ya Afrika Kusini

Akizungumzia siku hizo 10 nchini Afrika Kusini, Rweyemamu ameeleza kuwa mazingira mazuri na nidhamu ya wachezaji vilisaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha malengo ya benchi la ufundi.

“Ni kweli tulifika hapa tarehe 24, na leo ni siku ya 10. Kila kilichotuleta tumekimaliza. Zimekuwa siku kumi nzuri za mazoezi, umakini na mazingira rafiki yanayotuweka vizuri huko tunakoenda,” amesema Rweyemamu.

Ameongeza kuwa mapumziko ya kalenda ya FIFA yamewapa benchi la ufundi fursa adhimu ya kulijenga kikosi. Uwepo wa zaidi ya wachezaji 22 kambini ulimwezesha Kocha Steve Barker kutekeleza zaidi ya asilimia 90 ya mipango yake ya kitalaamu na kiufundi.

Matokeo ya Mechi za Kirafiki Siyo Kipimo cha Dabi

Wakiwa nchini Afrika Kusini, Simba SC ilicheza michezo miwili ya kirafiki (training games) dhidi ya Polokwane City na Sekhukhune United na kupoteza yote, ikiwemo ule wa mwisho uliomalizika kwa kufungwa mabao 2-1.

Hata hivyo, Rweyemamu amewatoa hofu mashabiki na kuweka wazi kuwa matokeo hayo hayawezi kuwa kipimo cha kiwango cha Simba kuelekea Dabi ya Kariakoo, kwani mechi hizo zililenga kupima mifumo na kuwapa wachezaji muda wa kucheza pamoja.

“Siyo mechi zinazotupa mwelekeo wa moja kwa moja, bali zilikua na lengo la kutoa nafasi kwa kila mchezaji kucheza, hata katika nafasi tofauti. Hiyo inaweza kuwa ilichangia matokeo, lakini katika mchezo wa mwisho kulikuwa na ushirikiano na mzunguko mzuri zaidi wa kikosi (rotation),” ameeleza.

“Umoja Wetu Ndio Nguvu Yetu” β€” Ujumbe Kwa Wanasimba

Kuelekea pambano la Oktoba 10, Rweyemamu anakiri kuwa Dabi ya Kariakoo haijawahi kuwa mechi rahisi, lakini amehakikisha kuwa kikosi kipo tayari kupambana na kusaka alama tatu muhimu.

Ametuma wito maalum kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wa Simba kote nchini kuungana pamoja katika kipindi hiki muhimu:

“Ratiba inayofuata ni Dabi. Mechi si rahisi, lakini hatuna jinsiβ€”tunaenda kupambana kupata matokeo. Tuende tukaungane, umoja wetu ndiyo nguvu wetu. Tuende tukaipeleke tarehe 10 kuhakikisha tunashinda mchezo huo.”

De Reuk Aipigia Yanga Mkwara Mzito: “Tuko Tayari Kwa Dabi ya Kariakoo!” Ahmed Ally Afunguka Kipigo cha Afrika Kusini: “Bora Tuumie Hapa!”