Ahmed Ally Afunguka Kipigo cha Afrika Kusini: “Bora Tuumie Hapa!”
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amefunguka kuhusu matokeo ya mechi mbili za kirafiki walizocheza nchini Afrika Kusini na kusisitiza kuwa hayajaingiza hofu yoyote kwenye kikosi hicho.
Simba SC ilicheza michezo miwili ya kujipima nguvu dhidi ya Polokwane City na Sekhukhune United ikiwa sehemu ya kambi yao ya siku 10 nchini humo. Kambi hiyo ililenga kujiweka sawa kabla ya kurejea kwa ratiba ngumu ya Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA.
Akizungumzia vipigo hivyo, Ahmed Ally alisema Simba haijutii hata kidogo kupoteza mechi hizo, kwani lengo kuu lilikuwa ni benchi la ufundi kubaini mapungufu halisi ya timu kabla ya kuingia kwenye mechi za ushindani.
βKwanza tunafurahi tumepoteza. Ni vizuri ukaumia katika uwanja wa mazoezi kuliko ujipatie majeraha kwenye uwanja wa vita. Ukitaka upate raha kwenye uwanja wa mazoezi, kuna hatari ukaja ukaumia zaidi kwenye mechi za ushindani. Majeraha tunayoyapata hapa si kitu,β alisema Ahmed Ally.
Akaongeza kuwa mechi hizo zilitumika kama kioo cha kuonyesha ukweli wa kikosi chao badala ya kudanganywa na matokeo ya kujiweka sawa:
βUkiruhusu mechi ya kirafiki ikudanganye, basi mechi ya kimataifa yenyewe itakuja kukuonyesha ukweli mbaya. Kwa hiyo, michezo hii ya Afrika Kusini imetutahadharisha na kutuonyesha ukweli mapema.β
Matokeo hayo sasa yanampa Kocha Steve Barker picha kamili ya maeneo yanayohitaji marekebisho ya haraka ili kukiweka kikosi hicho tayari kwa mapambano yanayowakabili mbele yao.