Ligi Kuu Bara Leo: Mechi Tatu Moto Kupigwa Mikoani, Vita ya Pointi Tatu Kusuka au Kutengua
LIGI Kuu Bara inarejea leo kwa mechi tatu zitakazopigwa katika mikoa mitatu tofauti, huku kila timu ikisaka pointi tatu muhimu katika kuendeleza malengo yake ya msimu wa 2026/27.
Mashujaa FC vs Polisi Tanzania (Saa 8:00 Mchana – Kigoma)
Mchezo wa mapema utapigwa katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, ambapo wenyeji Mashujaa FC watawakaribisha Polisi Tanzania.
Mashujaa itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na lengo la kuendeleza rekodi yake nzuri nyumbani, ambako imeshinda mechi mbili na kupata ushindi mmoja ugenini. Katika mechi sita ilizocheza hadi sasa, Mashujaa imeshinda tatu na kupoteza tatu. Timu hiyo inarejea uwanjani baada ya kutumia mapumziko ya ligi ya takriban wiki tatu kufanya maandalizi ya kina.
Hata hivyo, Mashujaa itahitaji kuwa makini katika safu yake ya ulinzi, kwani katika ushindi wake wa mechi tatu, imecheza mchezo mmoja pekee bila kuruhusu bao (cleansheet) ilipoichapa Coastal Union 1-0 ugenini. Kwa upande mwingine, Polisi Tanzania itapaswa kuwa makini na safu ya ushambuliaji ya Mashujaa inayoongozwa na Haroun Lyawatwa pamoja na Mishamo Daud.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Mashujaa, Amani Josiah, alisema:
“Tumerejea kwenye ligi baada ya mapumziko mafupi. Tumefanya maandalizi ya kutosha na tumeyafanyia kazi maeneo yaliyokuwa na mapungufu ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.”
Polisi Tanzania, ambayo msimu huu imerejea Ligi Kuu kwa kishindo, imeanza vyema kwa kushinda mechi tatu, sare moja, na kupoteza mbili. Rekodi hii inafanya mchezo wa leo kuwa wa kuvutia zaidi, kwani timu zote zimewahi kushinda ugenini msimu huu. Mashujaa itahitaji kumzuia mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Anoury Jabir, ambaye tayari amefunga mabao matatu katika mechi sita.
Kocha wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata, alibainisha kuwa wanatambua ugumu wa mchezo huo:
“Kucheza dhidi ya Mashujaa ni mchezo mgumu kutokana na ubora wa kikosi chao. Hata hivyo, tutajaribu kutumia makosa yao kutengeneza ushindi.”
Pamba Jiji vs Geita Gold (Saa 10:15 Jioni – Mwanza)
Mchezo wa pili utapigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ambapo wenyeji Pamba Jiji wataikaribisha Geita Gold.
Pamba Jiji inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na presha kubwa kutokana na matokeo yasiyoridhisha, baada ya kufungwa mechi tano na kupata sare moja pekee kati ya mechi sita ilizocheza. Matokeo hayo yamemuweka katika wakati mgumu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mkenya Francis Baraza, huku ushindi wa leo ukiwa ndio hitaji kuu la kuanza kugeuza mwenendo wa timu hiyo.
Kocha Baraza alisema:
“Tumekuwa na changamoto mbalimbali na tumeyafanyia kazi. Baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi wamerejea. Tunajua hautakuwa mchezo rahisi, lakini tunapambana tuweze kushinda.”
Geita Gold nayo haitakiwi kupuuzwa. Ingawa ilianza msimu kwa kasi kabla ya kupoteza mchezo wake wa mwisho ugenini dhidi ya Yanga SC, bado inabaki kuwa timu hatari. Kocha wa Geita Gold, Zuber Katwila, amesisitiza kuwa matokeo mabaya ya Pamba hayawapi nafasi ya kubweteka:
“Tunajua wenzetu hawana matokeo mazuri, lakini hilo halitufanyi tubweteke. Tumejipanga kukutana na mchezo mgumu na lengo letu ni kurudi kwenye njia ya ushindi.”
Namungo FC vs TRA United (Saa 1:00 Usiku – Lindi)
Mchezo wa mwisho wa siku utapigwa mkoani Lindi, ambapo wenyeji Namungo FC wataikaribisha TRA United. Mchezo huu pia unakutanisha makocha wanaofahamiana vyema—Juma Mgunda wa Namungo na Hemed Morocco wa TRA United, ambao waliwahi kufanya kazi pamoja kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Namungo imecheza mechi saba, ikishinda mbili na kupoteza tano, matokeo ambayo yameifanya timu hiyo kuwa katika nafasi isiyoridhisha. Kocha Juma Mgunda anaamini mapumziko ya wiki tatu yasiyokuwa na mechi yatawaletea mabadiliko chanya:
“Tumekuwa na mfululizo wa matokeo yasiyo mazuri, lakini katika wiki hizi tatu za mapumziko hatujatoka bure. Tunataka kuondoa hali hii haraka na kurudisha furaha kwa mashabiki.”
TRA United, chini ya Kocha Hemed Morocco, imeanza msimu vizuri baada ya kuichapa Pamba Jiji ugenini katika mchezo wake uliopita. Katika kipindi cha mapumziko, TRA United ilifanya kambi fupi Zanzibar na sasa inalenga kuendeleza kasi hiyo mjini Lindi.
Morocco, ambaye aliwahi pia kuifundisha Namungo FC, alisema:
“Namungo imekuwa ikikosa matokeo mazuri, lakini ni timu nzuri na ina kocha mzuri anayejua Ligi Kuu Bara vyema. Hii si mechi rahisi kabisa.”