Tiketi za Simba vs Yanga
Simba SC

Tiketi za Simba vs Yanga: Simba Yatoa Ukweli Kuhusu Tiketi za Kariakoo Dabi

Vardo October 8, 2026 12:59 pm

Wakati presha ya mchezo wa watani wa jadi kati ya Simba SC na Yanga SC ikizidi kupanda, sintofahamu kubwa imeibuka miongoni mwa mashabiki kufuatia kuchelewa kuanza kwa mauzo ya tiketi za mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wenyeji wa mchezo huo, Simba SC, wamejitokeza na kuweka wazi kuwa hawahusiki kwa namna yoyote na mchakato wa uuzaji wa tiketi hizo, huku wakitupa mpira huo mikononi mwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB).

Kwanini Mauzo ya Tiketi Yamechelewa?

Uongozi wa Simba umeeleza kuwa tofauti na misimu iliyopita ambapo klabu zilikuwa na mamlaka ya kusimamia mauzo ya tiketi zao, mfumo wa sasa hivi unaratibiwa kikamilifu na TFF pamoja na TPLB kupitia wazabuni wa mfumo wa kidijitali.

Licha ya viingilio vya mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kutangazwa rasmi, zoezi la ununuzi bado halijafunguliwa. Hatua hii imeleta presha kubwa kwa mashabiki, ikizingatiwa kuwa tiketi za mechi nyingine za ligi kuu tayari zimeanza kuuzwa.

“Tunapenda kuwataarifu mashabiki kuwa kwa sasa klabu haina mamlaka juu ya upatikanaji wa mzabuni wa tiketi kwa mechi zilizo chini ya TFF/TPLB. TFF ilitangaza tenda na tumetaarifiwa kuwa mchakato wa kumpata mzabuni umekamilika, lakini mpaka sasa uongozi haujapewa taarifa za mzabuni huyo,” ilieleza taarifa ya Simba SC.

Jitihada za Simba na Wito kwa Mashabiki

Ikiwa zimesalia siku chache kuelekea dabi hiyo ya Kariakoo, Simba imewatoa hofu mashabiki wake na kuwasihi kuwa na subira wakati wakisubiri mwongozo rasmi kutoka TFF.

Klabu hiyo imethibitisha kuwa tayari imechukua hatua za haraka kwa kufanya mazungumzo na mamlaka husika ili kupata suluhu ya haraka ya mfumo wa tiketi na kurahisisha zoezi la ununuzi kabla ya siku ya mchezo.

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa siku ya Jumamosi, Oktoba 10 katika Uwanja wa Uhuru, kuanzia saa 1:00 usiku.

Twiga Stars dhidi ya Botswana: Mbinu za Shime na Ratiba ya Mchezo wa Olimpiki 2028