Steve Barker Afichua Siri ya Ushindi wa Simba Dhidi ya Yanga Dabi ya Kariakoo
Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amevunja ukimya na kuweka wazi siri iliyoifanya timu yake kuibuka na ushindi mwembamba lakini wa thamani mkubwa wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga katika mchezo mkali wa Dabi ya Kariakoo.
Akizungumzia mchezo huo uliovuta hisa za mamilioni ya mashabiki wa soka nchini, Barker amesema kuwa mafanikio hayo hayakuja kwa bahati mbaya, bali yalisababishwa na moyo wa kupambana, nidhamu ya hali ya juu, na wachezaji wake kukataa tamaa hadi dakika ya mwisho.
Ushindi huo uliochezwa juzi umeleta hamasa kubwa na kurejesha furaha iliyopotea kwa mashabiki na wanachama wa Simba SC, ambao sasa wana kila sababu ya kutembea kifua mbele baada ya kuichapa Yanga katika pambano lililokuwa limejaa ushindani mkubwa, presha, na burudani ya soka.
Kocha huyo aliongeza kuwa anajivunia sana namna kikosi chake kilivyojituma uwanjani kwa pamoja kupigania nembo ya klabu hiyo na kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu muhimu dhidi ya watani zao wa jadi.
“Kilikuwa kiwango kizuri cha uchezaji, kilichojaa moyo na tabia ya kupambana. Ninajivunia juhudi zilizofanywa na wachezaji wangu katika mchezo huo. Nina furaha kubwa kuona mashabiki wetu wanaweza kusherehekea pointi tatu. Nguvu Moja!” alisema Barker.
Matokeo haya yanazidi kuongeza ushindani katika msimamo wa ligi na kuipa Simba SC nguvu mpya ya kuendelea na mapambano ya kusaka ubingwa msimu huu.