Kapombe Afunguka: Chilambo na Duchu Wataniweka Nje Simba SC?
NAHODHA na beki wa kulia wa Simba SC, Shomari Kapombe, amewamwagia sifa wachezaji wenzake katika nafasi hiyo, Nathaniel Chilambo na David Kameta ‘Duchu’, huku akieleza kuwa kiwango chao bora kinampa amani wakati akiendelea kujiweka sawa kurejea uwanjani.
Kapombe alikuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi miwili baada ya kupata jeraha baya la bega na mkono mwezi Agosti mwaka huu. Jeraha hilo lilimkuta wakati wa mashindano ya Kombe la Kagame yaliyofanyika Kigali, Rwanda, kufuatia kugongana na kipa wa timu hiyo, Hussein Abel.
Atia Neno Kuhusu Kurejea Uwanjani
Akizungumzia maendeleo ya afya yake pamoja na nafasi yake kikosini, Kapombe alisema kwa sasa yuko fiti na anaendelea vizuri, lakini uamuzi wa lini atacheza upo mikononi mwa kocha mkuu, Steve Barker.
“Ni jambo la kheri mimi niko mzima na ninaendelea vizuri. Kwa hiyo tunamuachia mwalimu (Steve Barker). Atakapoona nitakapofaa, basi nitacheza,” alisema Kapombe.
Maslahi Ya Simba SC Kwanza
Nahodha huyo alisisitiza kuwa jambo linalompa furaha zaidi si ushindani wa mchezaji mmoja mmoja, bali ni kuona timu inapata matokeo chanya kupitia wachezaji wanaopewa dhamana ya kucheza.
“Kama kiongozi wa wachezaji, mtu yeyote anapofanya kazi ndani ya uwanja na ikatupa mafanikio, mimi jambo langu la kwanza huwa ni kufurahi. Kitu cha kwanza ni timu, baada ya hapo ndiyo linakuja suala la mchezaji mmoja mmoja,” aliongeza.
Avutiwa Na Kiwango Cha Chilambo Na Duchu
Kapombe alihitimisha kwa kusema kuwa tangu Chilambo alipojiunga na klabu hiyo na Duchu kuendelea kupata nafasi ya kucheza, wote wameonyesha kiwango cha juu kinachostahili pongezi.
“Najivunia kuona wanaocheza katika nafasi yangu wanafanya vizuri. Najivunia na nasema wanaweza kuifanya Simba kufikia malengo yake,” alihitimisha Kapombe.