Yanga SC vs Kagera Sugar
Yanga SC

Yanga SC vs Kagera Sugar: Yanga Kusaka Pointi 3 Kurejea Nafasi ya Pili Ligi Kuu

Vardo November 1, 2026 8:50 am

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, leo wanatarajiwa kushuka dimbani katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, jijini Dar es Salaam, kuwakaribisha Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Yanga inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kiu ya kupata ushindi utakaoiwezesha kurejea katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo.

Msimamo wa Ligi Kuu na Hesabu za Yanga SC

Hivi sasa Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi 10. Ushindi wa leo utaifanya ifikishe pointi 25 na kuipiku Azam FC yenye pointi 23 (mechi 10), huku wajadi wao Simba SC wakiendelea kuongoza msimamo wakiwa na pointi 27 kutokana na michezo tisa.

Kauli ya Kocha Simon Dladla

Akizungumzia maandalizi ya kikosi hicho, Kaimu Kocha wa Yanga, Simon Dladla, amekiri kuwa Kagera Sugar haitakuwa mpinzani mwepesi kutokana na nafasi waliyopo kwenye msimamo.

“Tunatarajia mchezo mgumu leo kwa sababu tunakutana na timu inayopambana kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja. Tutapata upinzani mkubwa kama ule tuliokutana nao dhidi ya TRA,” alisema Dladla.

Pamoja na ugumu huo, Dladla amesisitiza kuwa lengo kuu la Wananchi ni kutetea ubingwa wao:

“Yanga ni timu kubwa yenye malengo makubwa. Lengo letu kuu ni kumaliza ligi tukiwa nafasi ya kwanza, na tutapambana kushinda kila mchezo uliosalia ili kufikia malengo hayo.”

Hamasa kwa Mashabiki na Uujio wa Sead Ramovic

Kocha Dladla pia amewaomba mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuongeza morali ya wachezaji wanapokusanya pointi tatu muhimu.

Mbali na ushindani wa uwanjani, mchezo wa leo unatarajiwa kuvuta hisia za wengi kwani mashabiki watapata fursa ya kumshuhudia kocha mpya wa timu hiyo, Sead Ramovic, akiwa na kikosi chake kipya baada ya kuchukua mikoba ya Manqoba Mngqithi.

Kapombe Afunguka: Chilambo na Duchu Wataniweka Nje Simba SC? Simba SC kuwakaribisha Namungo FC Uwanja wa Uhuru – Ligi Kuu