Siri ya Uhusiano wa Raheem Sterling na Paige Milian: Miaka 10+ Bila Ndoa
Winga wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza (England), Raheem Sterling, kwa miaka mingi amekuwa kwenye uhusiano thabiti wa kimapenzi na Paige Milian. Wawili hawa walifahamikana kabla hata Sterling hajapata umaarufu wala ukwasi unaotokana na soka la kulipwa.
Licha ya kucheza katika klabu kubwa nchini Uingereza zikiwemo Liverpool, Manchester City, Chelsea, na Arsenal, Sterling na Paige wamefanikiwa kulea familia yao na kupata watoto wawili, ingawa hadi sasa bado hawajafunga ndoa rasmi.
Uhusiano wao umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu na mashabiki pamoja na vyombo vya habari. Licha ya kuweka wazi baadhi ya mambo kwenye mitandao ya kijamii, wamefanikiwa kulinda mambo mengi ya familia yao kuwa siri.
Walivyokutana na Safari ya Mapenzi Yao
Paige na Sterling walikutana wakati nyota huyo akiwa kijana mdogo wa miaka 15 katika akademi ya Queens Park Rangers (QPR).
Muda mfupi baadaye, Sterling alijiunga na Liverpool. Hatua hiyo ilimfanya Paige kuacha kazi yake katika duka la vifaa vya michezo na kuhamia jijini Liverpool ili kuwa karibu na mpenzi wake. Hata hivyo, walipitia kipindi cha kutengana kabla ya kurudiana rasmi mwaka 2015, wakati Sterling akijiandaa kujiunga na Manchester City.
Paige amekuwa shahidi wa karibu katika kila hatua ya Sterling—tangu anaanza soka, aliposhinda mataji manne ya Ligi Kuu England (EPL) chini ya Pep Guardiola, mpaka alipopitia vipindi vigumu. Baada ya kucheza Arsenal kwa mkopo, Chelsea ilitangaza kusitisha mkataba wake mnamo Januari 2026, kabla ya kujiunga na Feyenoord ya Uholanzi kwa mkataba uliomalizika mwishoni mwa msimu wa 2025/26.
Posa, Ndoa Iliyokwama, na Familia
Machi 2018, Sterling alimchumbia Paige kwa kumvisha pete ya gharama kubwa ya almasi. Walipanga kufunga ndoa mwaka 2020, lakini mipango hiyo iliahirishwa kutokana na mlipuko wa janga la Covid-19, na mpaka sasa hawajatangaza tarehe mpya.
Hadi sasa, Paige anatambulika kama mchumba wa Sterling. Wawili hawa wamejaliwa watoto wawili wa kiume: Thiago (aliyezaliwa Januari 2017) na Thai (aliyezaliwa Mei 2019). Sterling pia ana mtoto wa kwanza wa kike, Melody Rose (aliyezaliwa Juni 2012), aliyepata na aliyekuwa mpenzi wake, Melissa Clarke.
Kwenye Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar—ambayo ilikuwa michuano ya mwisho kwa Sterling kuichezea England—nyumba yao ilivamiwa na majambazi Paige akiwa na watoto, jambo lililomfanya Sterling kurejea nyumbani kwa muda kuweka mambo sawa.
Ujasiriamali na Maisha Binafsi ya Paige Milian
Tofauti na wake au wapenzi wa wachezaji wengi (WAGs) wanaotafuta umaarufu, Paige ni mhasibu kitaaluma na mjasiriamali anayejisukuma mwenyewe.
Ye na Sterling ni wamiliki wa kampuni ya majengo ya Milian Property Group Limited, ambapo Paige ndiye mwanzilishi na mkurugenzi mkuu. Kwenye mitandao ya kijamii, anamiliki ukurasa wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya 100,000, ambapo mara nyingi hushirikisha mashabiki picha za familia na miradi yake ya kibiashara.