Miss Tanzania 2026
Burudani

Miss Tanzania 2026: Lamata Aweka Wazi Mabadiliko Makubwa, Kanda na Tarehe ya Fainali

Vardo November 1, 2026 9:49 am

Mashindano ya Miss Tanzania 2026 yanaendelea kuteka hisia za mashabiki wengi nchini, huku mwitikio mkubwa katika kanda mbalimbali ukirejesha heshima na mvuto wa mchuano huo tofauti na misimu iliyopita.

Safari ya msimu huu inaongozwa na Mkurugenzi Mpya, Leah Mwendamseke (Lamata), aliyekabidhiwa rasmi mikoba ya usimamizi Aprili 14, 2026, kutoka kwa Basila Mwanukuzi. Basila aliongoza mashindano hayo tangu mwaka 2018 alipopokea kijiti kutoka kwa marehemu Hashim Lundenga.

Chini ya uongozi wa Lamata, msimu wa Miss Tanzania 2026 ulizinduliwa rasmi Septemba 10 jijini Dar es Salaam ukiwa na kaulimbiu ya ‘Beauty for Positive Change’. Kaulimbiu hii inalenga kuunganisha urembo na maendeleo ya kijamii, uongozi, utamaduni pamoja na uwezeshaji wa wanawake.

Mwaka Huu Ni Tofauti: Ushindani Mkubwa Kwenye Kanda

Akizungumzia hatua iliyofikiwa, Lamata ameeleza kufurahishwa kwake na namna Watanzania walivyopokea mchakato wa mwaka huu, akimshukuru Mungu na kuwapongeza mashabiki kwa ushirikiano wao.

“Tofauti ya Miss Tanzania zilizopita na hii ni kwamba kuanzia kwenye kanda, washiriki na wasanii wamefanya shoo nzuri na kubwa sana. Nadhani hii ndiyo Miss Tanzania yenyewe,” alisema Lamata.

Mchakato wa mwaka huu unahusisha kanda saba (7):

  1. Kanda ya Kaskazini (Imekamilika)

  2. Kanda ya Ziwa (Imekamilika)

  3. Kanda ya Kusini (Imekamilika)

  4. Kanda ya Kati (Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma — Oktoba 31, 2026)

  5. Kanda ya Mashariki

  6. Kanda ya Dar es Salaam

  7. Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu

Sapraizi za Kutosha na Burudani Kanda ya Kati

Kuelekea kinyang’anyiro cha Kanda ya Kati, waandaaji wameahidi vitu vya tofauti vitakavyowashangaza mashabiki.

Mbali na shoo ya urembo, jukwaa litatwaliwa na burudani kutoka kwa wasanii nguli kama Nandy, Darassa, Stamina, na G Nako, huku Heroes Band ikiongeza msisimko wa mubashara kwa mashabiki watakaohudhuria.

Changamoto, Mvuto Kwenye Mitandao na Ukweli Kuhusu Msimu Huu

Kuhusu changamoto za uandaaji, Lamata alikiri kuwa ni mara yake ya kwanza kubeba jukumu la kitaifa la ukubwa huu, lakini changamoto hizo zimekuwa fursa ya kujifunza na kujenga uzoefu mpya.

Akijibu madai ya baadhi ya mashabiki kuwa mashindano yamepoteza mvuto kwenye mitandao ya kijamii, Lamata alipinga hoja hiyo na kuwataka mashabiki kuwa na subira:

“Naomba wasubiri waendelee kufuatilia hadi fainali ya Miss Tanzania ndipo watasema neno. Kwa sasa ni mwanzo tu, lakini Miss Tanzania mwaka huu ni kubwa na watajionea wenyewe.”

Washiriki 21 Kutinga Fainali Desemba 12

Katika msimu huu, jumla ya washiriki 21 pekee ndio watakaopenya kuingia fainali ya kitaifa. Kabla ya kumpata mshindi, warembo hao watapita kwenye mafunzo ya uongozi, mawasiliano, ziara za kiutamaduni na shughuli za kijamii.

Pia, safari yote ya washiriki itaonyeshwa kupitia vipindi 34 vya runinga vilivyosheheni utamaduni, mitindo na vivutio vya utalii.

Kilele cha mashindano hayo kinatarajiwa kufanyika Desemba 12, 2026, jijini Dar es Salaam, ambapo Mrembo mpya wa Tanzania atatawazwa rasmi.

Siri ya Uhusiano wa Raheem Sterling na Paige Milian: Miaka 10+ Bila Ndoa