Fadlu Davids: Yanga SC Hatutaki Robo Fainali Tena, Lengo Ni Ubingwa wa Afrika!
KOCHA wa Yanga SC, Fadlu Davids, amesema dhamira yake ni kubadilisha mtazamo wa klabu hiyo katika mashindano ya Afrika, akisisitiza kuwa lengo halipaswi kuwa kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika pekee, bali kupambana hadi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Fadlu amesema Yanga ni klabu kubwa yenye mashabiki wengi na wachezaji wenye uwezo, hivyo haina sababu ya kujiona duni inapokutana na vigogo wa soka la Afrika, akiwataka wachezaji wake kuwa na imani ya kushindana na timu yoyote bila kujali ukubwa au historia yake.
Kocha huyo amesisitiza kuwa licha ya Yanga kuwa katika Kundi B lenye Zamalek ya Misri, MC Alger ya Algeria na Club Africain ya Tunisia, kikosi chake hakipaswi kuingia uwanjani kikiwa na hofu, bali kiamini uwezo wake na kuendeleza falsafa ya kucheza soka la kutawala mchezo.
“Hatupaswi hata kwa sekunde moja kujiona sisi ni duni. Sitachukua mtazamo huo. Nitawafanya wachezaji waamini kwamba tunaweza. Tunatakiwa kuwa na busara zaidi tunapocheza ugenini, lakini bado tushikilie misingi yetu, mtindo wetu wa kucheza na kutawala mchezo,” amesema Fadlu.
Amesema wakati umefika kwa Yanga kubadili namna inavyojiwekea malengo katika mashindano ya Afrika, akieleza kuwa kufuzu hatua ya robo fainali hakupaswi kuwa mwisho wa safari, bali klabu hiyo inapaswa kuwa na dhamira ya kwenda mbali zaidi na hatimaye kulibeba taji.
“Huu ndiyo wakati wa sisi kutotaka tu kutoka kwenye kundi au kufika robo fainali na kuishia hapo. Tunatakiwa kubadili mtazamo wa klabu. Tusisherehekee sana tukivuka robo fainali, tunatakiwa kuwa na dhamira ya kulibeba kombe,” amesema.
Hata hivyo, Fadlu amesema malengo hayo yatafikiwa kwa hatua, akieleza kuwa kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha Yanga inafuzu kutoka hatua ya makundi kabla ya kuanza kuzungumzia robo fainali, nusu fainali na hatimaye fainali.
Katika Ligi Kuu ya NBC, kocha huyo amekiri kuwa hatma ya ubingwa haipo mikononi mwa Yanga kwa sasa, akieleza kuwa pamoja na kushinda michezo yote iliyosalia, bado wanahitaji timu zinazowatangulia kupoteza pointi ili waweze kurejea kileleni.
Amesema jambo la msingi kwa kikosi chake ni kuhakikisha kinapata ushindi katika kila mchezo uliosalia, ili kiwe tayari kutumia nafasi endapo wapinzani wao watafanya makosa na kupoteza pointi.
“Kile tunachoweza kufanya ni kushinda mechi zetu zilizobaki. Hata tukifanya hivyo bado tunatumaini wengine watapoteza pointi, lakini mara tu wanapopoteza pointi tunatakiwa tuwepo ili tuweze kurudi kileleni. Hilo ni muhimu sana,” amesema.
Mbali na Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika, Fadlu amesema Yanga bado ina dhamira ya kutwaa Kombe la CRDB, akisisitiza kuwa malengo ya klabu, rais wake na yeye kama kocha ni kuijenga timu itakayokuwa na uwezo wa kutawala soka la Afrika.
Akizungumzia nafasi ya vijana na wachezaji wazawa katika mipango yake, Fadlu amesema kundi hilo ni sehemu muhimu ya mradi wake, akieleza kuwa vijana wanahitaji kulelewa, kufundishwa na kupewa imani ili waweze kuonyesha uwezo wao na kufikia viwango vya juu.
Amesema tayari amegundua vipaji kadhaa katika mazoezi na anatamani kuviona vikikua hadi kupata nafasi katika kikosi cha kwanza, akisisitiza kuwa hataki kuwapa nafasi vijana kwa sababu ya kutimiza kanuni ya asilimia 10 ya wachezaji wanaotakiwa kuwa uwanjani, bali kutokana na imani aliyonayo katika uwezo wao.
“Vijana ndiyo kesho. Unatakiwa kuwalea, kuwafundisha, kuwapa kujiamini na kuwaonyesha kwamba wanaweza. Napenda sana kuwapa vijana nafasi. Tayari nimeona vipaji kwenye mazoezi na ninatarajia si tu kuwa nao, bali kuwavisha jezi kubwa,” amesema.
Katika hatua nyingine, Fadlu amesema kambi ya siku 10 ya Yanga visiwani Zanzibar ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kikosi hicho, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya michezo yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika itachezwa katika visiwa hivyo.
Amesema kambi hiyo itawasaidia wachezaji kuzoea mazingira ya Zanzibar, ikiwemo hali ya joto wakati wa mchana na muda wa kuanza kwa mechi, ili kuhakikisha mambo hayo hayawi kikwazo wanapokutana na wapinzani wao.
Ameongeza kuwa kipindi hicho pia kitampa nafasi ya kuweka misingi ya falsafa yake ya uchezaji, kuwaelekeza wachezaji namna anavyotaka timu icheze na kupata kiwango bora kutoka kwa kila mmoja.
Kuhusu kurejea kwa Ligi Kuu na michezo mikubwa ya dabi, ikiwemo Kariakoo dhidi ya Simba na Mzizima dhidi ya Azam FC, Fadlu amesema anatambua uzito wa mechi hizo kutokana na uzoefu alioupata katika dabi mbalimbali alizowahi kushiriki akiwa kocha.
Amesema aliwahi kuwa sehemu ya dabi ya Kaizer Chiefs dhidi ya Orlando Pirates nchini Afrika Kusini, pamoja na Wydad dhidi ya Raja nchini Morocco, hivyo anaelewa presha, ushindani na matarajio yanayoambatana na michezo hiyo.
Ameeleza kuwa moja ya faida alizonazo ni kuwafahamu wapinzani wake, akidai anajua maeneo ambayo wana nguvu na yale yenye mapungufu, jambo litakalomsaidia kuandaa kikosi chake kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.
“Ni dabi kubwa sana. Faida yangu ni kwamba nawajua wapinzani. Najua wapi ni dhaifu na wapi ni imara. Hizi ni mechi tunazopaswa kushinda. Tumezungumzia kushinda mechi zilizobaki na dabi zimo humo bila shaka,” amesema Fadlu.