Enock Morrison Yanga na Simba
Michezo Bongo

Mghana Enock Morrison Atamani Kucheza Simba na Yanga, Afunguka Kilichokwamisha Usajili Wake

Vardo November 14, 2026 8:18 pm

KIUNGO mshambuliaji hatari wa klabu ya Al-Merrikh SC ya nchini Sudan, raia wa Ghana, Enock Morrison, ameweka wazi kuwa ndoto na malengo yake makubwa kisoka ni siku moja kuvaa jezi za miamba ya soka nchini Tanzania, Yanga SC au Simba SC.

Morrison ametoa kauli hiyo katika mahojiano maalum aliyoyafanya nchini Sudan, akibainisha kuwa licha ya kupata ofa kutoka klabu ya Singida Black Stars mara baada ya kumaliza mkataba wake na Gor Mahia ya Kenya msimu wa 2025-2026, bado moyo wake unatamani kucheza Kariakoo.

Kilichokwamisha Dili Lake Kutua Simba SC

Nyota huyo amefichua kuwa alikuwa hatua chache tu kujiunga na Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, lakini mazungumzo hayo yalikwama dakika za mwishoni kutokana na kushindwa kufikia muafaka kwenye baadhi ya vipengele vya kimkataba.

“Yanga na Simba ni timu kubwa na zenye ushindani mkubwa kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Hilo linajidhihirisha kutokana na ubora wa wachezaji wakubwa kutoka mataifa mbalimbali wanaocheza hapo. Bado nina malengo ya kucheza Tanzania siku moja,” alisema Morrison.

Hali hiyo ya kushindwana na Simba SC pamoja na Singida Black Stars ndiyo iliyomfanya kiungo huyo kutimkia Sudan kujiunga na matajiri wa Al-Merrikh SC.

Rekodi ya Kipekee Aliyoiweka Kenya (MVP)

Enock Morrison, aliyezaliwa Januari 18, 2000, ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kucheza kama kiungo wa kati mshambuliaji (Namba 10) pamoja na kutokea pembeni (Winga). Kabla ya kutua Afrika Mashariki, aliwahi kuzitumikia klabu kubwa za kwao Ghana zikiwemo King Faisal FC na Asante Kotoko.

Katika msimu wa 2025-2026 akiwa na mabingwa wa Kenya, Gor Mahia (‘K’Ogalo’):

  • Alichangia jumla ya mabao saba (7) katika mechi 31 alizocheza (akifunga mabao 3 na kutoa pasi za mabao/assists 4).

  • Aliiwezesha Gor Mahia kutwaa ubingwa wao wa 22 wa Ligi Kuu ya Kenya.

  • Alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu (MVP), na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kushinda tuzo hiyo nchini Kenya baada ya kupita miaka 14, akivunja rekodi iliyowekwa na Mganda Dan Sserunkuma mwaka 2012.

Meridianbet Yaleta Mwanga Wa Tumaini Tandale