Simba na Kamati ya Uchaguzi ya TFF
Simba SC

Simba Yagomea Majibu ya TFF Kwenye Vyombo vya Habari, Yatishia Kwenda Mahakamani!

Vardo November 15, 2026 11:28 pm

DAR ES SALAAM: Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba SC imepinga vikali utaratibu uliotumiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wa kujibu hoja zao kupitia vyombo vya habari, ikisisitiza kuwa mawasiliano ya kiofisi yanapaswa kujibiwa kwa maandishi.

Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa leo Novemba 15, 2026, uongozi wa Simba umebainisha kuwa mnamo Novemba 13, mwaka huu, uliwasilisha barua rasmi kwa TFF ukielezea msimamo wao kuhusu mwenendo wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo, sambamba na kutoa mapendekezo ya maboresho na kuomba majibu rasmi.

Hata hivyo, Bodi hiyo imeeleza kusikitishwa na hatua ya Mwenyekiti huyo kukimbilia kwenye vyombo vya habari kujibu hoja hizo kabla ya kuipatia klabu majibu ya barua yao, ikisema kitendo hicho hakizingatii misingi ya uongozi na taratibu za mawasiliano ya taasisi zinazosimamia soka nchini.

Simba Yakanusha Kuwepo kwa ‘Simba Mbili’

Katika hatua nyingine, klabu hiyo imekemea vikali kauli zinazodai kuwa ndani ya Simba kuna makundi mawili yanayokinzana—yakihusishwa na ofisi ya mwekezaji iliyopo Masaki na ile ya Mwenyekiti Mzee Murtaza Mangungu iliyopo Msimbazi. Simba imeonya kuwa kauli hizo zinaweza kupotosha umma na kuleta athari za kisheria.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa Simba SC ni taasisi moja imara inayoongozwa na Katiba moja ya mwaka 2018 (iliyofanyiwa marekebisho Novemba 30, 2025 na kusajiliwa rasmi Februari 18, 2026). Hivyo, wanachama na mashabiki wameombwa kupuuza madai ya uwepo wa “Simba mbili” na kutambua kuwa kuna mfumo mmoja tu wa kiuongozi.

Hatua za Kisheria na Wito kwa Wanachama

Aidha, Simba imethibitisha dhamira yake ya kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa uhuru, haki, na uwazi kwa kuzingatia Katiba ya klabu, Kanuni za Uchaguzi za TFF, pamoja na miongozo ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Wakati huohuo, jopo la wanasheria wa klabu hiyo linaendelea kupitia kauli za Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF ili kuchukua hatua stahiki za kisheria.

Mwisho, Bodi ya Wakurugenzi imewasihi wanachama, mashabiki, wadhamini, na wadau wote wa Msimbazi kuendelea kuwa watulivu na kudumisha umoja wao katika kipindi hiki ambacho viongozi wanashughulikia suala hilo.

Ahmed Ally Atamba Baada ya Abdul Razaq Hamza Kurejea Simba: “Orlando Pirates Waje Tu, Jeshi Limekamilika!”