Rasmi: Kocha Simon Dladla Aondoka Yanga na Kutua Richards Bay FC
Aliyekuwa kocha msaidizi na kaimu kocha mkuu wa klabu ya Yanga, Simon Dladla, ametangaza rasmi kuachana na mabingwa hao wa soka Tanzania na kurejea nchini kwao Afrika Kusini baada ya kukubali kibarua kipya cha kuinoa klabu ya Richards Bay FC inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo (PSL).
Kupitia ujumbe mzito aliouchapisha kwenye ukurasa wake rasmi wa Instagram, Dladla ameushukuru uongozi wa Yanga kwa kumpa fursa ya kuitumikia klabu hiyo yenye historia kubwa barani Afrika, kwanza kama kocha msaidizi wa kwanza na baadaye kumwamini kukaimu nafasi ya kocha mkuu.
“Kufanya kazi ndani ya klabu kubwa yenye historia kama Yanga imekuwa heshima kubwa kwangu na hatua muhimu katika safari yangu ya ukocha. Nimefurahia sana ushirikiano na mazingira niliyokutana nayo wakati wote nilipokuwa Dar es Salaam,” ameeleza Dladla.
Sababu ya Kuondoka Jangwani
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amebainisha kuwa uamuzi wake wa kuondoka umetokana na mwelekeo mpya wa kiufundi ambao uongozi wa Yanga umeuchukua. Amesema anaamini ni jambo la msingi kumpa kocha mkuu mpya pamoja na benchi lake la ufundi uhuru kamili wa kutekeleza falsafa na mipango yao bila kuingiliwa.
“Nimekubali changamoto mpya ya kuwa kocha mkuu wa Richards Bay FC nyumbani Afrika Kusini,” amethibitisha Dladla katika taarifa yake.
Shukrani kwa Uongozi wa Yanga
Aidha, Dladla ametoa shukrani za dhati kwa viongozi wa juu wa Yanga, akiwemo Rais wa klabu, Makamu wa Rais, Mtendaji Mkuu (CEO) pamoja na wajumbe wote wa Bodi ya Wakurugenzi kwa weledi, sapoti na ukarimu mkubwa waliompa katika kipindi chote alichokuwa klabuni hapo.
Amemalizia kwa kusisitiza kuwa Yanga itaendelea kubaki kuwa sehemu maalumu moyoni mwake, akieleza kuwa milango ipo wazi na yupo tayari kutoa huduma zake endapo klabu hiyo itamhitaji tena siku zijazo, huku akiitakia kila la kheri katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.