Usajili wa Fei Toto Simba
Simba SC

Usajili Mpya Simba: Fei Toto Kutua Msimbazi, Kiungo Huyu Kutolewa Kama Chambo Azam FC

Vardo November 20, 2026 8:36 am

Uongozi wa klabu ya Simba SC umeripotiwa kuingia katika hatua nzito za mazungumzo na mabosi wa Azam FC kwa lengo la kukamilisha usajili wa Fei Toto Simba (Feisal Salum) katika dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Taarifa za kuaminika zilizolifikia Soka la Bongo zinaeleza kuwa wekundu hao wa Msimbazi wamedhamiria kwa dhati kuinasa saini ya kiungo huyo mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, ambaye kwa sasa ni tegemeo kubwa ndani ya kikosi cha matajiri wa Chamazi, Azam FC.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, Simba SC ipo tayari kutoa kitita cha fedha ili kupata huduma ya nyota huyo. Hata hivyo, katika hali inayozidi kunogesha dili hilo, Azam FC nayo imeonyesha kuvutiwa na kiungo wa Simba, Inno Juspin Loemba, na imependekeza ajumuishwe kama sehemu ya makubaliano ya uhamisho huo.

Pendekezo lililopo mezani kwa sasa ni Simba kutoa kiasi cha fedha pamoja na kumwachia Loemba aelekee Chamazi, huku uongozi wa Msimbazi ukielezwa kutokuwa na pingamizi lolote endapo hatua hiyo itafanikisha lengo lao kuu la kumpata Fei Toto.

“Ni kweli tuna uhitaji mkubwa wa huduma ya Fei Toto na mazungumzo yaliyopo kwa sasa ni kwa ajili ya kumpata katika dirisha dogo. Makubaliano yetu ni kutoa kiasi cha fedha, lakini wao wanahitaji huduma ya Loemba, hilo kwetu hatuna pingamizi,” kilieleza chanzo hicho.

Endapo mazungumzo baina ya pande hizo mbili yatafikia mwafaka, Simba SC itakuwa imelamba dume kwa kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kupitia ubunifu wa Fei Toto, huku Azam FC ikipata mbadala wa haraka kupitia ujio wa Loemba. Hadi sasa, hakuna klabu yoyote kati ya hizo iliyotoa taarifa rasmi juu ya mwenendo wa mazungumzo hayo.

Tetesi za Usajili: Yanga Yarudi Tena kwa Kiungo Alphonce Mabula Rasmi: Kocha Simon Dladla Aondoka Yanga na Kutua Richards Bay FC