Ratiba Kombe la Dunia U-17 Qatar 2026 Leo: Italia, Senegal na Mali Vitani
Msisimko wa michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17 (Qatar 2026) unaendelea kushika kasi leo Novemba 20, 2026, ambapo mechi nyingine nane kali za hatua ya makundi zitapigwa. Jumla ya mataifa 16 yatashuka dimbani kusaka alama muhimu katika fainali hizi za kihistoria zinazoshirikisha timu 48.
Kundi E: Mabingwa wa Ulaya Italia Kuanza Kazi Dhidi ya Jamaica
Macho ya mashabiki wengi yatakuwa katika Kundi E litakalowakutanisha mabingwa wa Ulaya U-17, Italia, dhidi ya Jamaica, huku Ivory Coast ikipimana nguvu na Uzbekistan.
Italia inaingia katika mashindano haya ikiwa na morali ya juu baada ya kutwaa taji la Ulaya mwaka huu kwa kuifunga Ubelgiji kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1. Kwa upande wao, Jamaica si timu ya kubeza kwani ilifuzu kwa kishindo ikishinda mechi zote tatu za ukanda wa Concacaf na kufunga mabao 18, ikiongozwa na nahodha wao hatari, Jahmarie Nolan, aliyefunga mabao manne na kutoa asisti mbili.
Katika mchezo mwingine wa kundi hilo, Ivory Coast inasaka kufuta machungu ya mwaka jana ambapo ilipoteza mechi zote tatu za makundi. Hata hivyo, wababe hao wa Afrika Magharibi wana historia nzuri ya mwaka 1987 walipomaliza washindi wa tatu. Watakabiliwa na kibarua kigumu mbele ya Uzbekistan iliyofuzu baada ya kutinga nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Asia U-17, ikijivunia vipaji vya nyota wake Asilbek Aliev na Muhammad Khakimov.
Kundi F: Senegal Kuwakilisha Afrika, Cuba Yarejea Baada ya Miaka 35
Katika Kundi F, mabingwa wa Afrika U-17 mwaka huu, Senegal, watavaana na Croatia, huku Cuba ikimenyana na Tajikistan.
Senegal inashiriki fainali hizi kwa mara ya nne ikiwa na lengo la kuvuka mafanikio yake ya mwaka 2019 na 2023 ilipoishia hatua ya 16 bora, kabla ya kutolewa hatua ya 32 bora mwaka 2025. Wakati huo huo, Cuba inaweka rekodi ya kipekee kwa kurejea kwenye fainali za Kombe la Dunia U-17 baada ya kupita miaka 35 tangu iliposhiriki mara ya mwisho mwaka 1991. Mshambuliaji Yankarlos Iglesias anatazamiwa kuwa tegemeo lao baada ya kuchangia mabao mawili na asisti moja katika hatua ya kufuzu.
Kundi G: Mali Kufufua Makali ya 2015, Ubelgiji Kukipiga na Vietnam
Kundi G litashuhudia vigogo wa soka la vijana Afrika, Mali, wakiumana na New Zealand, wakati wanafainali wa Ulaya, Ubelgiji, wakikutana na Vietnam.
Mali, ambao waliwahi kucheza fainali mwaka 2015 na kushika nafasi ya tatu na ya nne katika matoleo mengine, wanaingia wakiwa na kiu ya kufanya makubwa zaidi baada ya kuishia hatua ya 16 bora mwaka jana. Watakutana na New Zealand ambayo rekodi yake bora ni kufika hatua ya 16 bora mwaka 2009, 2011 na 2015. Ubelgiji nayo inaanza kampeni yake ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza fainali ya Ulaya kwa penalti dhidi ya Italia, ikitaka kudhihirisha ubora wake mbele ya Vietnam.
Kundi H: Hispania Kusaka Taji la Kwanza, Morocco Kuikabili Fiji
Katika Kundi H, Hispania itakuwa na kibarua dhidi ya China, huku Fiji ikikutana na wawakilishi wengine wa Afrika, Morocco.
Hispania inaingia ikiwa na rekodi ya kucheza fainali nne za Kombe la Dunia U-17 (1991, 2003, 2007 na 2017) bila bahati ya kubeba kombe, hivyo mwaka huu inasaka kuvunja mwiko huo. Upinzani wao utatoka kwa China iliyomaliza nafasi ya pili kwenye Kombe la Mataifa ya Asia U-17 nyuma ya Japan, ikitegemea ubora wa beki Junior Zamorano na kiungo Zhou Yunuo.
Kwa upande wa Morocco, inaingia dimbani ikiwa na uzoefu mkubwa wa kufika robo fainali katika matoleo mawili yaliyopita (2023 na 2025). Mshambuliaji Ziyad Baha anabaki kuwa silaha kuu ya Simba wa Atlas baada ya kufunga mabao manne mwaka jana, yakiwemo mawili kwenye ushindi mnono wa 16-0 dhidi ya New Caledonia. Fiji inayoshiriki kwa mara ya pili mfululizo itamtegemea zaidi kiungo wake mzoefu na nahodha wa mwaka jana, Maikah Dau.