MANCHESTER, ENGLAND: NYOTA kadhaa wa sasa na wa zamani wa Manchester City pamoja na wake na wapenzi wao walionekana wakiburudika usiku manane kwenye sherehe ya kuwaaga mastaa wa kikosi hicho, Bernardo Silva na John Stones.
Kiungo Silva ataondoka Man City majira ya kiangazi baada ya miaka tisa klabuni, huku nyota kama Phil Foden na mkewe Rebecca Cooke wakihudhuria kumuaga nahodha huyo pamoja na Stones aliyesajiliwa 2016.
Nahodha wa zamani wa Man City, Kyle Walker, aliyeichezea timu hiyo kati ya 2017 hadi 2025 kabla ya kuhamia Burnley naye alikuwepo ingawa hakuonekana na mkewe Annie Kilner. Inaelezwa kuwa timu hiyo ilikusanyika katika klabu ya usiku ya Louis Night Club katikati mwa Jiji la Manchester na sherehe hiyo ilidumu kwa saa tano na nusu. Mastaa waliwasili saa mbili usiku na wa mwisho kuondoka saa 1:30 asubuhi.
Kiungo Mateo Kovacic aliwasili akiwa na mkewe Izabel, huku kipa wa England, James Trafford na nyota wa zamani wa Arsenal, Kolo Toure, ambaye ni sehemu ya benchi la Pep Guardiola pia wakihudhuria.
Silva alisafirishwa nyumbani na mwenzake Ruben Dias kwa kutumia gari la kifahari aina ya Lamborghini Urus 4×4, licha ya nyumba yake kuwa umbali wa mita chache kutoka eneo la sherehe. Inadaiwa mmoja wa wafanyakazi wa hoteli walipokuwa amesema: “Sidhani kama alikuwa na uwezo wa kutembea (kutokana na kuzidiwa kilevi).”
Foden aliyekuwa amevaa shati jeupe, jinzi na koti la bluu aliondoka kabla ya saa nne usiku akiwa na Rebecca, mama wa watoto wake watatu.
Marc Guehi alionekana akiondoka saa 10:30 alfajiri huku Erling Haaland akiwa ameambatana na mpenzi wake Isabel Haugseng Johansen pia walikuwepo. Badala ya kupiga picha, wawili hao walijificha ndani ya gari la kifahari aina ya Maybach Mercedes S Class lenye thamani ya Pauni 400,000. Wachezaji wengine waliondoka kwa kutumia magari yenye vioo vyeusi kupitia mlango wa nyuma. Marcus Bettinelli, Nicolas Gonzales, Matheus Nunes, Rayan Ait Nouri, Abdukodir Khusanov, Tijjani Reijnders, Nathan Ake na Rodri wote walihudhuria.
Stones na mkewe Olivia Naylor hawakuonekana, lakini picha za hafla hiyo zilikuwa na maandishi “Bernardo and John.” Mke wa Reijnders, Marina, aliweka picha mtandaoni akiwa pamoja na mumewe, Silva, Nathan Ake na wake zao huku akiambatanisha na emoji sita za moyo wa bluu.
Usiku huo ulikuwa wa kusherehekea mafanikio ya Silva aliyeshinda mataji 18 akiwa City yakiwemo Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu England. Hata hivyo, City bado wanapambana kutwaa taji la saba la ligi wakiwa na Silva. Hivi karibuni waliifikia Arsenal kileleni baada ya ushindi dhidi yao mwezi uliopita, lakini sare dhidi ya Everton, Jumatatu, ilirudisha faida kwa Arsenal. Arsenal sasa wanaongoza kwa pointi tano huku zikiwa zimebaki mechi tatu wakati City walio nafasi ya pili bado wana mechi nne.