Home Uncategorized WAZAWA JIPIMENI KWENYE SURA YA JOHN BOCCO

WAZAWA JIPIMENI KWENYE SURA YA JOHN BOCCO


Na Saleh Ally

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo sasa, Simba tayari wanakwenda kwenye usajili ambao utawalazimisha kuangalia kilicho sahihi zaidi.

Wakati Simba wakiangalia kilicho sahihi lazima watakuwa wanapanda kutoka hatua moja kwenda nyingine kwa maana ya ubora zaidi katika msimu ujao.

Kwa nini Simba wanahitaji kawa bora zaidi? Jibu ni kwa kuwa wameona makosa yao mengi sana wakati wakiwa katika Ligi Kuu Bara ambayo mwisho wameibuka kuwa mabingwa. Lakini wameona makosa mengi sana wakati wakishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ligi ya Mabingwa Afrika walifika katika hatua ambayo kwa muongo mzima au miaka ya hivi karibuni hawakuwa wamefikia katika hatua hiyo. Safari hii wamefikia hatua ya robo fainali ambayo ina ugumu wa juu ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Baada ya kufika katika hatua hiyo watakuwa wamejifunza mengi sana na hasa hatua ya makundi ambayo tuliona, Simba ilionekana dhaifu kiasi cha kufungwa mabao 12 katika mechi tatu tu.

Kama wastani maana yake walifungwa mabao manne kila mchezo bila ya wao kufunga hata moja lakini uhalisia unaonyesha walifungwa 5-0 mara mbili na mwisho 2-0. Hivyo wanajua wanahitaji kipi hasa.

Bila ubishi Simba wanahitaji wachezaji bora kabisa wenye kiwango kilicho sahihi ambacho kitawafikisha mbali zaidi na kuwafanya kuwa na timu imara hata ikitoka nje ya Tanzania badala ya kuwa na kikosi chenye ubora wa juu kinapokuwa nyumbani peke yake.

Ukiangalia sababu kuu iliyowang’oa ni kutokuwa imara nje ya nyumbani kwani baada ya TP Mazembe kufanikiwa kuizuia Simba nyumbani na kuilazimisha sare, basi wakawa wamemaliza kila kitu kwa kuwa wakati Simba inaondoka kwenda Lumbumbashi, hakuna aliyekuwa na matumaini ya ushindi kule DR Congo.

Kwa nini hakuna matumani? Jibu Simba haikuwahi kushinda ugenini katika kiwango hicho, badala yake hatua ya awali iliposhinda dhidi ya Mbabane Swallows. Sasa Simba inahitaji kuwa ina uwezo wa kushinda nyumbani katika kiwango cha juu zaidi ya hicho ilichokuwa nacho lakini inahitaji kushinda ugenini angalau uwezo wa uhakika wa saizi ya kati.

Haya yatawezekana kama Simba itakuwa na kikosi imara. Kikosi hicho lazima kiundwe na wachezaji bora, makocha bora kwa maana ya yule wa makipa, wa viungo, kocha msaidizi na bosi wa benchi lenyewe. Tayari wanao lakini kikubwa ni suala la kupima.

Wakati tunakwenda huko, huu ndiyo wakati mzuri wa kujitathmini kwa wachezaji wa hapa nyumbani Tanzania. Kama wachezaji wazalendo, nani anajiona yu sahihi kuweza kugombea namba au kupata nafasi Simba ambayo inafikiria ukubwa au nguvu zaidi?

Kawaida timu iliyokuwa na mafanikio zaidi na hasa kama imehusisha Bara, inaweza kuwa kipimo cha wachezaji wa nchi husika. Kwamba wanapata nafasi kiasi gani na waliopo nje ya kikosi hicho wanaweza kushindana na walio ndani ili kuiimarisha Simba.

Kiwango cha kuwaza cha Simba, kitakuwa ni nje ya Tanzania. Ukitengeneza timu bora inayoweza kushindana kiwango cha Bara la Afrika, bila shaka itakuwa na uwezo wa kushiriki vizuri ligi ya ndani.

Wachezaji wazawa hawa walio Simba hawakuwa na nafasi kubwa sana kama wageni. Angalia, mchezaji pekee ukiachana na kipa Aishi Manula unaweza kusema alikuwa vizuri sana ni John Raphael Bocco.

Nahodha huyo wa Simba ni mfano wa kuigwa na ubora wake umekuwa mchango katika kuendesha timu, kuzalisha mabao na ikiwezekana yeye mwenyewe kufunga. Achana na hivyo, angalia uchezaji wake wa juhudi, maarifa na mfano ambao hata ukimuuliza mchezaji yeyote mgeni lazima amtaje Bocco.

Bocco amekuwa mshindani wa namna, mshindani uwanjani na kiongozi sahihi. Wachezaji wengine wa Kitanzania hili limewashinda na viwango vyao vilikuwa ni vile vya kupanda na kushuka na wakati mwingine kunaweza kuwa na kisingizio cha wageni lakini kama kiwango chako ni bora, hakuna wa kukuzuia kama ambavyo Bocco ameonyesha.

Walio ndani ya Simba wanalijua hilo lakini hata walio nje bila ya ubishi watakuwa wameliona hilo na liko wazi. Nani anatamani kuwa kama Bocco au madai ya wachezaji kama Erasto Nyoni au Mohammed Hussein Zimbwe ambaye baada ya kurejesha kiwango chake kikaendelea kupanda siku hadi siku?

Kwa kipindi hiki Simba inasaka wachezaji wa kuifanya iwe bora zaidi, basi kikubwa walitakiwa jicho lao liwe Tanzania zaidi. Lakini ninaamini bado watalazimika kuwaacha wageni na kuongeza wageni tena kwa kuwa Watanzania walikuwepo lakini bado hawakuwa na ushindani bora zaidi au ubora unaoendelea.

Kuna jambo la kujifunza. Tuache kulalamika sana kwa kuwa ukiwa mlalamishi sana, unapoteza utulivu wa kukupeleka katika njia sahihi ya kufanya kinachotakiwa katika wakati mwafaka. Kubali makosa, jifunze na uwe wewe mpya.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA NYUMA GAZETI LA SPOTI XTRA ALHAMISI