YANGA, AZAM KUTOANA MACHO KWA MKONGOMANI HUYU…OYA JAMAA SIO POA AISEE..
KATIKA harakati za kuboresha kikosi kwa ajili ya msimu ujao, inaelezwa kwamba Yanga ipo katika mawindo ya winga Mkongomani, Henoc Molia, huku ikibainisha imeingilia dili la Azam ambayo nayo ilikuwa na hesabu za kumshusha pale Chamazi.
Ikumbukwe kuwa, Azam ilipokea ripoti ya awali kutoka kwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Florent Ibenge, kwamba katika mastaa ambao anawahitaji Chamazi msimu ujao winga Henoc Molia ni miongoni mwao.
Klabu hizi mbili zote zimeendelea kujenga vikosi vya msimu ujao kimya kimya, lakini wamejikuta wakitaka mchezaji mmoja na wote wanahitaji huduma yake msimu ujao.
Henoc ni miongoni mwa wachezaji waliotolewa kwa mkopo kutoka FC Rangers kwenda Lupopo, lakini Azam ilipotua DR Congo ilienda moja kwa moja klabu ambayo anaichezea kwa sasa na kufanya mazungumzo.
Yanga ilipopata taarifa kwamba Azam imefika Lupopo kumsaka Henoc na ikapata uhakika kwamba sio mchezaji wa klabu hiyo, walienda mbali zaidi mpaka kwenye timu yake ya FC Rangers.
Baada ya kuwasiliana nao, ndipo ikatuma ofa kujaribu kama watafanikisha hesabu za kumchukua winga huyo anayewindwa na Azam FC pia.
HESABU ZA YANGA
Mpaka sasa kikosi hicho kina idadi kamili ya wachezaji wakigeni 12 ambao wanahitajika kikanuni, lakini mabosi wa klabu hiyo tayari wameshapiga hesabu za nani anatoka ili kumpisha Henoc kama atapatikana.
Pale Jangwani wachezaji wa kigeni wanaocheza nafasi hiyo ni Celestine Ecua ambaye alishatolewa kwa mkopo kwenda JS Kabylie ya nchini Algeria.
Lakini ndani ya Yanga yuko Maxi Nzengeli ambaye anaupiga mwingi na bado ana mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu hiyo, ila hesabu za kuondoka zimetua kwa Buba Jameh.
Mgambia huyo alitua Yanga dirisha dogo la Januari 2026, lakini kiwango chake kimeonekana kutowaridhisha mabosi wa klabu hiyo na yeye ndiye anatajwa atampisha Mkongomani huyo msimu ujao kama Yanga itaizidi kete Azam.