Home Uncategorized YALIYOTOKEA MSIMU HUU YASIJIRUDIE KESHO, WACHEZAJI WAFUNDISHE ‘FAIR PLAY’ UWANJANI

YALIYOTOKEA MSIMU HUU YASIJIRUDIE KESHO, WACHEZAJI WAFUNDISHE ‘FAIR PLAY’ UWANJANI

LIGI Kuu Bara imeisha kiubishi kwa kuwa tumeshuhudia namna ilivyokuwa inakwenda kwa mwendo wa kuchechemea ila mwisho wa siku mshindi kapatikana.

Simba anapaswa pongezi kwa kutetea ubingwa wake msimu huu kwani haikuwa rahisi kufikia malengo ambayo amejiwekea hivyo ni muda mwingine mzuri kwake kujipanga kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Msimu huu alifanya vizuri kwa kutinga hatua ya robo fainali hivyo msimu ujao wachezaji wanapaswa wawe na hasira zaidi ya mafanikio na kutinga hatua ya nusu fainali ili kuongeza thamani yao.

Licha ya ligi kuisha bado mapungufu mengi yameonekana ambapo yamekuwa yakiua ule utamu wa soka letu ambao ulianza kunoga mwanzo wa ligi katikati ukakata moja kwa moja.

Ni muda mwafaka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujipanga upya na kuangalia namna bora itakayoondoa makosa ambayo yameonekana msimu huu.

Kwa kuanza waanze na ratiba hasa kwenye mpangilo wanapaswa wawe safi mwanzo mwisho bila kujitia doa kama ambavyo imekewa msimu huu ambao umefika tamati.

Kila timu inapaswa ijipange kutimiza ratiba kwa wakati bila kujiwekea vikwazo vya moja kwa moja, kwa mfano ipo wazi kwa sasa Simba itacheza michuano ya Ligi ya Mabingwa itapendeza kama itakumbuka hili na kuchungulia mambo yalivyokuwa msimu huu.

TFF wana mawasiliano mazuri na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ni rahisi kwao kupata ratiba ya michuano ya Afrika itakavyokuwa hata kwa mtindo wa rafu kwani kila kitu kinawezekana ili kuepuka yaliyotokea msimu huu.

Ikumbukwe kwamba msimu huu kuna timu nyingi zilikuwa na viporo ambavyo havina hata ulazima jambo ambalo lilichangia kuua ushindani wa ligi yetu ambayo inazidi kupiga hatua.

Hivyo msimu ujao tunatarajia mabadiliko makubwa na utendaji makini sio kujirudia tena makosa ambayo yamefanyika msimu huu kwenye ligi.

Pia kwa sheria ambazo huwa zinawekwa zifuatwe pamoja na kanuni isiwe wanaweka wao wenyewe kisha wanazipuuzia hili halipo sawa kama ilivyo kwenye viporo msimu ujao vipunguzwe ama kutokuwepo kabisa.

Ligi bora inaendeshwa na waamuzi makini duniani hakuna timu ambayo inaweza kuwa bora kama itakuwa inabebwa ama kufanya vitendo ambavyo vinatoa viashiria vya kubebwa hakuna.

Hivyo waamuzi waache kuchezesha wakichanganya mapenzi yao ya klabu ama maamuzi yao binafsi sio sawa, tumeona msimu huu kuna baadhi ya marefa wanaingia uwanjani na matokeo mfukoni.

Hili ni doa ambalo limetibua ligi msimu huu ni lazima lisafishwe msimu ujao ili kufanya uwe wa tofauti na wa kipekee katika timu zote zitakazoshiriki pamoja na wahusika wote ambao watashiriki.

Kila mmoja atimize majukumu yake kwa wakati na kuanza kujipanga ni sasa kabla ya msimu mpya kuanza hapo baadaye, nina imani kupitia ripoti pamoja na yale ambayo yamejitokeza msimu huu itakuwa histora msimu ujao.

Jambo jingine ni kwa wachezaji wenyewe kujifunza namna ya kujali wachezaji wenzao hasa wawapo uwanjani ni kitu cha msingi kuliko hata matokeo yenyewe.

Kwa sasa kumekuwa na maumivu mengi kwenye soka hasa kutokana na kuripotiwa baadhi ya wachezaji wakipoteza maisha wakiwa ndani ya uwanja hvyo ni muhimu kujali kwa wachezaji.

Endapo inaweza kutokea tukio ambalo labda mwamuzi hajaona ama wachezaji hawajaona itakuwa ni hatari kwa timu nzima pamoja na mchezaji mwenyewe.

Hivyo jambo la msingi wachezaji wote wanapaswa wajue kwamba mlinzi wa mchezaji mwingine ni mchezaji mwenyewe uwanjani.

Kama linatokeoa tatizo anapaswa atoe huduma kwanza kabla ya kuangalia matokeo ambayo anayapa kipaumbele kwani uhai wa mchezaji ni bora muda wote kuliko matokeo yenyewe.

Itakuwa ni wakati mzuri pia kwa timu zote kujifunza kuwa na ‘Fair Play’ uwanjani ili kutoa mwanya kwa wachezaji kuwa na maamuzi sahihi kuhusu afya za wachezaji.

Ikitokea hivyo itawajengea uwezo wachezaji kujali na kuwa na maamuzi yenye busara wawapo uwanjani kwenye mashindano muda wote.

Kwa kufanya hivyo pia kutaokoa maisha ya mchezaji ambaye amepatwa na matatizo akiwa ndani ya uwanja bila kujali yupo mazingira gani ilimradi naye pia ni mchezaji.

Soka sio mchezo wa maumivu bali ni mchezo wa uungwana kwa kila mmoja ndio maana wachezaji wamekuwa wakipeana mikono ikiwa na maana kwamba wote ni kitu kimoja.

SOMA NA HII  SAFU YA ULINZI YA SIMBA YATAFUTIWA DAWA NA SVEN