Home Uncategorized MAVUGO NA YANGA MAMBO SAAAAAFII

MAVUGO NA YANGA MAMBO SAAAAAFII


IMEFAHAMIKA kuwa mabosi wa Yanga wapo kwenye mazungumzo ya mwisho ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Napsa Stars FC ya nchini Zambia, Laudit Mavugo aliyewahi kuichezea Simba.

Yanga chini ya Kocha Mkuu wa timu hiyo Mkongomani, Mwinyi Zahera wamepanga kukisuka kikosi cha timu hiyo ili msimu ujao wa Ligi Kuu Bara wauchukue ubingwa wa ligi unaoshikiliwa na Simba.

Timu hiyo tayari imekamilisha usajili wa wachezaji tisa ambao ni kipa Farouk Shikalo, Maybin Kalengo, Issa Bigirimana, Lamine Moro, Patrick Sibomana, Erick Rutenga, Abdul Aziz Makame, Ally Ally na Ally Sonso.

Huyu atakuwa ni mchezaji wa kulipwa ‘profeshno’ wa saba kutua Yanga katika kipindi hiki cha usajili.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu kutoka kwa rafiki wa karibu wa mshambuliaji huyo, mabosi wa Yanga tayari wamemfuata Mavugo na kama mazungumzo yakienda vizuri na wakifikia muafaka mzuri, basi atasaini.

Mtoa taarifa huyo alisema, Mavugo ambaye aliwahi kuichezea Simba atasaini Yanga baada ya kuwepo kwenye orodha ya washambuliaji ambao kocha Mwinyi Zahera anawahitaji katika kikosi chake.

Aliongeza kuwa, mabosi hao tayari wamefanya mawasiliano na mshambuliaji huyo atakayecheza pacha na mshambuliaji wa Zesco, Kalengo ambaye tayari amesaini mkataba wa miaka miwili Yanga.

“Yanga imemfuata Mavugo kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya awali ili wamuongeze katika usajili wao wa msimu na kama mazungumzo yakienda vizuri, basi atasaini miaka miwili.

“Kocha ndiye aliyetoa mapendekezo ya kumsajili baada ya kujadiliana na msaidizi wake, Mwandila (Noel) ambaye ni raia wa Zambia anayeifuatilia ligi ya nchini huko, akiamini ataisaidia Yanga kwenye msimu ujao.

“Mavugo ni kati ya washambuliaji tishio hivi sasa Zambia, hivyo kama Yanga wakifanikiwa kumsajili, basi watakuwa na kikosi tishio msimu ujao wa ligi,” alisema rafiki yake huyo raia wa Burundi.

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela kuzungumzia hilo alisema:

“Kocha ameacha orodha yake ya wachezaji anaowahitaji kusajiliwa kwa uongozi ambayo tunaendelea kuifanyia kazi.

“Na tulichopanga ni kusajili mchezaji yeyote atakayemhitaji katika usajili wake na hilo linawezekana na nisingependa kuweka wazi huyo mshambuliaji yupo au hayupo kwenye orodha yake ya usajili, kikubwa ni kuvuta subira.”

SOMA NA HII  BARCELONA SASA KUMUUZA NYOTA WAO GRIEZMANN ILI KUPATA MKWANJA