UONGOZI wa Simba umesema kuwa klabu ya Polokwane FC ya nchini Afrika Kusini imekiuka makubaliano ya FIFA kwa kudai mchezaji John Bocco ni mali yao.
Jana Simba walitoa taarifa rasmi kuhusu kumuongezea kandarasi ya miaka miwili nahodha wa kikosi hicho John Bocco ghafla wameibuka viongozi wa timu ya Polokwane wakidai mchezaji ni wao.
Polokwane wamedai kwamba Bocco alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo yenye maskani yake Afrika Kusini.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori amesema kuwa klabu hiyo imekiuka makubaliano ya FIFA kwa kumsainisha mkataba mchezaji mwenye mkataba.
“Hata kama mchezaji amebakisha miezi sita ni lazima klabu iandikiwe barua ili kupata taarifa, mchezaji alisema amesaini mkataba wa awali, ndio maana tukamsainisha.
“Wao hawajaandika barua kwa ajili ya kutaka kumsainisha mchezaji Bocco, niliongea na wakala wa aliyemsainisha mkataba, hivyo niliwaambia kwamba wamekiuka makubaliano ya mkataba ndio maana hata TP Mazembe walipotaka kumsainisha mkataba Ajibu walituma barua kwa Yanga
“Huwezi kumsainisha mkataba mchezaji mwenye mkataba ndani ya mkataba hivyo hao wanaosema wamemsainisha mkataba Bocco wamekiuka makubaliano ya FIFA,” amesema Magori.