UONGOZI wa Azam FC leo umemtangaza rasmi kocha Etienne Ndayiragije aliyekuwa KMC kuwa kocha wao mpya kwa msimu wa 2019/20.
Akizungumza mara baada ya kutambulishwa, Ndayiragije amesema kuwa sababu kubwa iliyomuondoa KMC ni maamuzi yake binafsi pamoja na maisha ya soka kutokuwa ya kudumu sehemu moja.
“Nimefanya kazi kwa ukaribu na KMC, ni watu wangu wa karibu sina tatizo nao ila maisha ya soka ni kutafuta changamoto mpya na sio tatizo la fedha, mfano kocha Guardiola aliondoka Barcelona hakukuwa na tatizo na bado anaendelea na kazi yake hivyo hivi ndivyo maisha ya soka yalivyo.
“Najua nipo kwenye kikosi bora kwa sasa nitapambana kuendelea kufanya kazi yangu kwa kushirikiana na wengine kwani nafasi ya kufanya kazi ipo na tunaweza kufanya vizuri,” amesema Ndayiragije.