TIMU ya taifa ya mpira wa kikapu ya wanaume na wanawake imewaomba watanzania kuwachangia fedha ili iweze kumudu gharama za kwenda Uganda kushiriki mashindano ya Kanda ya Tano (FIBA Zone V) yaliyopangwa kufanyika Juni 25 mwaka huu.
Timu hiyo inatarajiwa kuondoka tarehe 23 na wachezaji 24, makocha wawili kila timu, madaktari na viongozi wa TBF ambapo idadi yao inafikia 33 na wanahitaji kiasi cha Sh. milioni 57 ili kufanikisha safari hiyo ambapo kiasi hicho kitatumika kwenye kuwasafirisha, kuwapatia malazi, chakula na posho za wachezaji na viongozi.
Rais wa TBF Phares Magesa amesema “Tunaomba Watanzania watusaidie michango yao ya hali na mali kwa sababu tunatakiwa kwenda Uganda kushiriki mashindano ya (FIBA Zone V) ambayo yatatusaidia kupata tiketi ya kwenda kushiriki mashindano ya FIBA Afrika.
“Wachezaji wote wapo tayari kwa mashindano ila kikwazo ni kupata pesa kwa ajili ya safari hiyo, hivyo kwa yeyote ambaye atataka kutuma chochote anaweza kutuma kupitia namba 0715 969567,” amesema.