Home Uncategorized FURAHA YA TAIFA IMEBEBWA NA TIMU YA TAIFA KWA SASA WACHEZAJI PAMBANENI

FURAHA YA TAIFA IMEBEBWA NA TIMU YA TAIFA KWA SASA WACHEZAJI PAMBANENI


GANZI ambayo wanayo watanzania kwa sasa ni kuanza vibaya kwenye michuano ya Afcon hasa ukizingatia kwamba imepita miaka 39 bila timu yetu kushiriki.

Hakuna wa kumlaumu kwa sasa kutokana na namna ambavyo tumeanza  na aina ya kikosi ambacho tulipambana nacho ambacho ni Senegal.

Ukitazama namna mabao 2 waliyotufunga namna yalivyopatikana ilikuwa ni patashika kidogo kwa kila mchezaji kupambana ila mwisho wa siku tulipoteza.

Tumeona namna ambavyo kila mmoja amekuwa akitimiza majukumu yake lakini yale makosa madogo ndiyo ambayo yametugahrimu.

Kuna jambo la kujifunza kwenye mchezo wetu wa kwanza hasa katika namna ya kuokoa mipira ya hatari ambayo inakuwa karibu na eneo la hatari.

Benchi la ufundi linapaswa liongee na wachezaji kwamba kwa sasa tunacheza na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kufanya maamuzi ya haraka kwa wakati sahihi.

Hivyo hilo litawafanya wachezaji kuwa makini mara mbili zaidi ya awali kama ilivyokuwa mwanzo kwenye mchezo wa kwanza ambao hatukuwa na namna ya kushida zaidi ya kupoteza mchezo wetu.

Ipo wazi kwamba kwa sasa hatuna uwezo wa kutwaa ubingwa wa Afcon kutokana na namna halisi ya mpira wa miguu ulivyo na ushindani.

Haina maana kwamba sipendi kuona Bendera ya Taifa letu inapepea na kufanya maajabu hapana ila sayansi ya mpira kwa sasa inatukataa.

Ushindani ambao tunaonyesha bado unatupa nafasi ndogo kutwaa ubingwa licha ya kwamba kwenye mpira chochote kinaweza kutokea.

Ukweli ni kwamba kwa sasa kikosi chetu kimekwenda kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao hasa baada ya kupata uzoefu kenye michuano hii mikubwa.

Kazi kubwa ya wachezaji uwanjani kama ambavyo nilisema awali kwamba wanapaswa wafungue zaidi akili zao na kucheza kimataifa tofauti na vile ambavyo wamezoea.

Kwa sasa mashindano haya hayahitaji mazoea ama urafiki hapa ni mwendo wa kupambaa kiukweli bila kukata tamaa.

Haina maana kwamba vijana wetu wanashindwa kupambana hapana wakati mwingine tunapaswa tuliangalie na benchi la ufundi namna linavyowapa majukumu vijana wetu.

Ipo wazi kwamba mbinu kubwa ambayo tunaitumia kwa sasa kwa timu ya Taifa ni kujilinda zaidi huku tukishambulia kwa kushtukiza hiki ndicho kinachotokosesha ushindi.

Kwenye mchezo wa mpira kikanuni kama timu itatumia mbinu ya kujilinda inapaswa iwe na uhakika wa kutumia vizuri nafasi ambazo wanazipata bila kufanya makosa ili kuendelea kupaki basi.

Pia mbinu hii imekuwa ikitumia kwa timu ambayo inalinda matokeo ambayo imepata hivyo inapaswa benchi la ufundi lijiulize linalinda ushindi upi mwanzo mwisho bila kufunguka?

Matokeo ya kushindwa iwe ni somo kwetu na kuangalia namna bora ya kufanya vizuri wakati mwingine kwenye mechi nyingine ambazo zinafuata.

Kwa sasa Taifa kwa karibu linafuatilia michuano hii ambayo inaendelea nchini Misri hivyo ni muda wetu kufanya vizuri na kupata matoke chanya.

Benchi la ufundi linapaswa likae chini na kufanya tathmini upya kwa kupitia makosa ambayo yameonekana kwenye mchezo wa kwanza.

Ule usemi wa mpira ni mchezo wa makosa usipuuzwe hasa kwa kila idara kutumia nafasi yake ipasavyo kwa kujilinda na kushambulia jambo litakalotupa nafasi ya kusonga mbele zaidi.

Ushindi hauwezi kupatikana kama timu itajilinda muda wote hakuna miujiza katika hili ni lazima timu ifunguke na ifanye mashambulizi.

Raha ya mpira ushindi na furaha ya mashabiki imejificha kwenye matokeo chanya, watanzania tusikate tamaa kama ambavyo wachezaji wetu wanapaswa wakumbuke kwamba wanapeperusha Bendera ya Taifa.

 Kila kitu kinawezekana na wachezaji jukumu lenu ni kupambana kwa ajili ya Taifa hilo msisahau na onyesheni nidhamu ndani na nje ya uwanja.

Tunawaamini wapambanaji basi msituangushe katika hili ambalo mmepewa jukumu zito la kufanya kwenye michuano hii ambayo tayari imeanza kunoga.

SOMA NA HII  HUYU HAPA AMEONGEZEKA KILO 10 YANGA, KAZI ANAYO