Home Uncategorized YANGA AMUENI, KINDOKI ANASTAHILI AONDOKE, SHIKALO NA WATANZANIA ITAWEZEKANA

YANGA AMUENI, KINDOKI ANASTAHILI AONDOKE, SHIKALO NA WATANZANIA ITAWEZEKANA



Na Saleh Ally
YANGA imeanza maandalizi ya msimu mpya ikijiandaa katika kambi yake ambayo iko mjini Morogoro kwa siku kadhaa sasa.


Kambi hiyo imekuwa ikiendelea vizuri kutokana na kwamba pamoja na mazoezi lakini Yanga imekuwa ikicheza mechi kadhaa za kirafiki kujipima.


Kitu kikubwa ambacho wanatakiwa kuongeza Yanga ni mechi ngumu zaidi kwa ajili ya kuendelea kukiinua na kukichambua kikosi chake kwa kuwa mechi ngumu, husaidia kujua upungufu wa mambo kulingana na kiwango.


Kuanza na mechi nyepesi ni jambo sahihi, hili linaruhusiwa kitaalamu kwa kuwa timu inatakiwa kuibuka taratibu na si sahihi kuanza na mechi ngumu maana unaweza kusababisha majeraha kwa wachezaji ambao wanakuwa bado hawajawa tayari.



Yanga ipo kambini Morogoro ikiwa na makipa watatu ambao wataisaidia timu hiyo wakati wa msimu ujao. Wawili kati yao ni wageni na mmoja kinda, Ramadhani Kabwili ndiye Mtanzania.

Farouk Shikalo raia wa Kenya, kipa ambaye kazi yake kabla ya kutua Yanga imeonyesha atakuwa na msaada na mwingine ni Klaus Kindoki ambaye amekuwa na Yanga msimu uliopita na suala la kiwango chake, haliwezi kuwa geni tena.


Kiwango cha Kindoki hakikuwa cha kuridhisha hadi kufikia kusema Yanga inamhitaji sana kwa kiwango cha juu sana. Mara kadhaa nimekuwa nikieleza kwamba Yanga inapaswa kumuacha Kindoki aondoke zake kwa heshima.


Tuliona namna Kabwili alivyolazimika kuokoa jahazi licha ya kwamba Yanga ilimsajili kama kinda na kipa wa baadaye. Kutokana na kiwango “kilicholala” cha Kindoki, Kabwili akalazimika “kukuzwa” kwa haraka naye akawa shujaa wa Yanga katika mechi kadha wa kadha.


Kwa maana ya ubora hajaitendea Yanga haki, hakuwa ni mchezaji ambaye alistahili kutokea nje ya Tanzania akaichezea Yanga. Kiwango chake, Yanga ingeweza kupata hapa kwa wachezaji wa ndani na ikiwezekana hata zaidi yake.


Kuonyesha kuwa kweli Kindoki hakuwa na kiwango ambacho Yanga walikihitaji, unaona wamemsajili Shikalo. Kama angekuwa anaweza na anategemewa, Yanga isingehangaika kumsajili kipa mwingine wa kimataifa.


Kutua kwa Shikalo, maana yake lazima Kindoki aondoke. Kitaalamu au kiuhalisia, Yanga haistahili kuwa na makipa wawili wa kigeni. Hii si sawa kwa ajili ya Yanga na mpira wa Tanzania.


Tunapaswa kukumbushana kwamba Yanga ni klabu ya Tanzania, tena ni klabu yenye historia ndefu zaidi unapozungumzia mpira wa Tanzania kuliko nyingine yoyote. Inahusika na mengi kuhusiana na nchi hii likiwemo suala la uzalendo.


Vizuri kujipima katika hili, kwamba kwa klabu kubwa kama Yanga, yenye timu kongwe hapa nchini, inastahili kuwa na wachezaji wa kigeni 10, halafu wawili wakawa makipa?
Binafsi nitasema hapana, ninaamini wengi watasema hapana. Kwamba yule ambaye ni mgeni anastahili hasa kuwa namba moja, baada ya hapo mmoja wa makipa bora Tanzania lakini pia Kabwili.


Kwa umri wake Kabwili ataendelea kukua, kipa mwingine Mtanzania ataendelea kushirikiana na kujifunza kupitia Shikalo ambaye pia ni kipa wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.


Hakuna ubishi kuwa Tanzania ina makipa wengi sana. Si kwa Yanga pekee lakini klabu zote za Tanzania, hazipaswi kuwa na wachezaji wawili wa kigeni katika namba moja. Lazima kuwe na mgeni ambaye atachuana na wenyeji nasi tukuze mpira wetu.


Kindoki huenda ni mtu mwema sana na asiye na matatizo kabisa, lakini uwepo wake Yanga ni kazi na kiwango kimeshamshitaki. Hivyo hakuna mjadala hata kabla ya Shikalo kutua, yeye alitakiwa kuwa ameondoka zake kwa kuwa Yanga wanachotaka kwake ni ufanisi.


Lazima tujifunze kwamba wakati tunaangalia kwa ajili ya klabu zetu, tusijisahau kuhusiana na taifa letu. Sisi ni Watanzania na tunapaswa kuwa wazalendo kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza, Tanzania ndio kwetu na hatuwezi kuhama.


Hivyo kuendelea kubaki na Kindoki ni kudhulumu nafasi ya wachezaji wa Kitanzania bila sababu za msingi. Yanga msikubali kuingia kwenye dhambi ya dhuluma hiyo, badala yake mna muda wa saa kadhaa kulifanyia kazi hili.


Nina imani siku ya utambulisho wakati wa kilele cha Wiki ya Mwananchi, Yanga mtatangaza kipa mmoja tu mgeni, wengine wawe wazalendo kwa ajili ya Yanga na Tanzania kwa kuwa ndipo ilipo Yanga.

SOMA NA HII  YANGA YAPIGA HESABU KUWEKA REKODI MPYA KARUME LEO