Home Uncategorized KADI ZA NJANO 1,200 ZA WAAMUZI ZILIVYOTULIZA MZUKA LIGI KUU ENGLAND

KADI ZA NJANO 1,200 ZA WAAMUZI ZILIVYOTULIZA MZUKA LIGI KUU ENGLAND


NA SALEH ALLY
NGUVU ya Ligi Kuu England maarufu kama EPL imepanda kwa kiasi kikubwa msimu uliopita kwa mara ya kwanza kukiwa na uthibitisho wa wazi kuwa ni ligi bora zaidi ya nyingine za mchezo wa soka duniani.

Ukiachana na sifa kadhaa ambazo imekuwa ikipewa ligi hiyo kama vile ugumu, kasi, nguvu na kadhalika, lakini suala la fainali zote mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League kuwa “mali ya England”, lilimaliza ubishi.

Maana Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa Liverpool dhidi ya Tottenham huku Arsenal wakiwavaa Chelsea katika Europa League. Makombe hayo mawili yalishatua nchini England hata kabla ya fainali hizo mbili kuchezwa.

Bila shaka ubora wa Ligi Kuu England unatokana na aina ya uchezaji, ubora wa wachezaji wenyewe na makocha. Lakini mpangilio bora wa viwanja vyao, namna ya kuingia na mvuto unaowafanya watu kwa wingi wazidi kuamini soka ni burudani na biashara.

Ubora unaozungumziwa hauwezi kuwa katika kiwango cha juu sana kama kutakuwa hakuna waamuzi bora wanaoifanya kazi hiyo.

Maana ili kuongeza ushindani sahihi unaotengeneza ubora, lazima kuwe na waamuzi bora hasa. Waamuzi ambao wanachezesha soka katika kiwango sahihi kinachohifadhi nidhamu na usahihi wa mambo.

England pamoja na kwamba waamuzi wake wengi wa kati hawapati nafasi kubwa katika michuano ya Uefa, lakini uhalisia unaonyesha kuna waamuzi ambao wanafanya kazi yao vizuri.

Pilika za uchezaji wa England kama mwamuzi hayuko sahihi, basi kila kitu kinavurugika na hasa suala la nguvu na kasi ya uchezaji wa timu 20 za ligi hiyo.

England ligi yake imeongezeka utani kwa kuwa hakuna timu ndogo katika mechi haujui nani ataibuka na ushindi. Iko hivi lazima usubiri matokeo hadi mwisho ndiyo uweze kusema.

Mwamuzi wa England anapaswa kuwa fiti kweli na hii inasababisha wengi wao kuwa wakali na kuwa na kiwango kikubwa cha utoaji wa kadi hasa za njano.

Kadi nyekundu kwa England zinaweza zikawa hazitoki kwa wingi sana, lakini njano zimekuwa zikimwagwa kama njugu ili kupunguza presha ya aina ya uchezaji wa Kingereza.

Mwamuzi Mike Dean msimu uliopita wa 2018/19 alichezesha mechi 29 za EPL na kuwa mmoja wa waamuzi waliochezesha nyingi. Aliyeongoza alikuwa na mechi 32, waliofuatia wana 29.

Katika mechi 29 za Dean, alitoa kadi 128 za njano na kuongoza kuwa mwamuzi aliyemwaga kadi nyingi za njano kwa msimu huo. Kama haitoshi, Dean akatoa kadi 10 nyekundu na kuongoza pia.

Ukiangalia ni jumla ya kadi 29 nyekundu zilitolewa kwa msimu mzima na Dean akawa na tano, akichukua kipande kikubwa cha utoaji wa kadi.

Kadi za njano jumla zilitoka 1,221, hivyo kuifanya Ligi Kuu England kuwa moja ya ligi zenye kadi nyingi za njano kwa msimu mmoja.

Dean anajulikana kuwa mmoja wa waamuzi wasio na masihara, yeye ni sehemu ya kuifanya EPL kuwa bora na inaonekana kuwa ligi hiyo ina nyota wengi na inafanya waamuzi kuwa katika wakati mgumu kama hawatakuwa makini.

Mambo mawili magumu kwa waamuzi ni nyota wanaofanya nao kazi wakati wakipambana lakini ukubwa wa klabu. Ubora na umaarufu wa England pia unachangia kuwa na timu nyingi kubwa na maarufu.

Manchester United, Liverpool, Manchester City, Arsenal, Chelsea, Tottenham na nyingine na hii inasababisha ligi hiyo kuwa na mechi nyingi kubwa.

Ukiachana na Dean kuongoza kumwaga kadi nyingi nyekundu na njano akiwa na jumla ya kadi 138, Anthony Taylor anafuatia kwa kuwa na kadi 101 za njano lakini msimu wote alitoa kadi moja tu nyekundu ya moja kwa moja maarufu kama ‘straight’.

Kevin Friend amechezesha mechi 27, akamwaga kadi 93 za njano sawa na Jonathan Moss lakini Friend ana nyekundu tatu na Moss ana 5, moja ikiwa straight na nne muunganiko wa njano na nyekundu.

Katika waliofikisha kadi za njano zaidi ya 90, wamo Martin Atkinson mwenye 91, Craig Pawson mwenye 92 lakini Michael Oliver mwenye 83, pia Paul Tierney mwenye 82.

Wingi huu wa kadi katika mechi 380 za msimu mzima, unaonyesha kuna ugumu wa kuchezesha EPL na waamuzi wakati mwingine wanalazimika kuwa wakali sana.

Kiwango kinachotakiwa ni kutokuwa na makosa ili kuweka umakini na haki. Malalamiko yakizidi yanapoteza mwelekeo wa ligi husika na hili, limepewa kipaumbele sana kwa kuwa FA ya England inatambua waamuzi ni kiungo muhimu na ubora wao ni chachu ya mafanikio.

Kumbuka, EPL haiweki rundo la waamuzi katika mechi hizo 380 ili iwe rahisi kusimamia ubora, ndiyo maana ni waamuzi 18 tu wa kati wanaochezesha msimu mzima.

SOMA NA HII  KINACHOENDELEA BAINA YA YANGA NA FALCAO - VIDEO